Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Daruso), imeshangazwa na kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii kwa barua ya kumsimamisha masomo mwanafunzi wake Abdul Nondo, badala ya kumkabidhi mwenyewe.
Hata hivyo, Rais wa Daruso Jeremiah Jilili, ameikosoa barua hiyo kuwa na makosa mengi ikiwamo kukosewa kwa kozi anayosoma Nondo lakini pia haikuwa na muhuri kuonyesha uhalali wake.
Barua ya kusimamishwa kwa Nondo iliyosainiwa na Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa William Anangisye, ilianza kusambaa jana Jumatatu saa tatu usiku, ikielezea kumsimamisha kwa sababu ya kuwa na kesi ya kutoa taarifa za uongo katika mitandao na kudanganya kutekwa, ambapo kutokana na sababu hizo Nondo atarudishwa chuoni baada ya kumalizika kwa kesi hiyo.
Jilili amesema hata yeye barua hiyo ameiona kwenye mitandao ambapo aliwasiliana na Ofisi ya Mshauri wa Wanafunzi kwa sababu ndiyo mtu anayehusika na uhusiano wa wanafunzi ambapo amemjibu ana taarifa za barua hiyo na amepelekewa nakala.
“Nikamuuliza ni kwanini barua hiyo kwanza haina muhuri halafu imeandikwa College of Humanity idara ambayo haihusiani na Nondo ambaye anasoma Social Science, akanijibu hiyo imeshabadilishwa.
“Lakini nikamwambia ni kwanini imewekwa kwenye mitandao wakati lengo la hiyo barua si kuwekwa kwenye mitandao kama hivyo kwa sababu ile inamhusu mhusika na si umma akasema zile barua ziko mbili ya kwanza ni ile inayoonekana kwenye mitandao ya pili imeelekezwa kwa Nondo na Ofisi ya mshauri wa Wanafunzi na watu wengine wanaostahii kupata barua hiyo, lakini barua zote zinazotakiwa kwenda sehemu husika zimeshafika zinakoelekezwa,” amesema.
Aidha, akifafanua hatua watakazochukua baada ya Nondo kusimamishwa masomo, amesema suala hilo ni kwa mujibu wa sheria za chuo ambazo zinasema kwamba mtu ukiwa na kesi ya jinai au ukifunguliwa mashtaka unasimamishwa, ndiyo maana Nondo hajafukuzwa chuo ila amesimamishwa.
“Sasa ukizingatia kesi yenyewe iko mahakamani ni suala ambalo halihitaji kuzungumziwa kwa mujibu wa katiba.
“Sisi kuna namna ambayo tulijaribu kulifuatilia tangu mwanzo kwa maana ya kutumia utawala na mawasiliano na polisi na vitu kama hivyo, lakini sasa kwa hapo tulipofikia hapo kesi ya Nondo ikishaisha kwa mfano Nondo akishinda anarudi chuoni na akishindwa sijajua utaratibu unakuwaje,” amesema.
Kwa upande wake Ofisa Habari wa TSNP, Helen Sisya amesema wanachama wa mtandao huo na yeye binafsi hawajaiona barua hiyo na Nondo bado hajafika chuoni hivyo hajakabidhiwa.
“Hata sisi tunasikia tu kwenye mitandao, tumesikia Profesa amethibitisha na kama amethibitisha sawa, hatuwezi kusema lolote.
“Lakini hizo hatua ni kwa mujibu wa sheria ndogo za chuo zinaruhuzu hivyo kwamba mwananfunzi akiwa na kesi ya jinai mahakamani anasimamishwa chuo, lakini unaweza kuona kuwa ni sheria mojawapo kandamizi kwa hiyo mimi kwa sasa naomba nisiseme lolote hadi niongee na wenzangu tuone tunafanyaje,” amesema Helen.