Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) jana imezindua rasmi utoaji wa vitambulisho vya Wafanyabiashara wadogo walio kwenye sekta isiyo rasmi ikiwa ni pamoja na Wamachinga.
Akizungumza wakati wa hafla fupi ya uzinduzi huo iliyofanyika jijini Dar es Salaam, Kamishna Mkuu wa Mamlaka hiyo Charles Kichere alisema kuwa, utoaji wa vitambulisho kwa wafanyabiashara wadogo unatokana na marekebisho ya Sheria ya Usimamizi wa Kodi ya Mwaka 2015 yaliyofanywa na Bunge la Bajeti la Mwaka wa Fedha 2017/2018 ambapo moja ya marekebisho hayo ni kuwatambua na kuwapatia vitambulisho maalum wafanyabiashara wadogo walio kwenye sekta isiyo rasmi.
“Baada ya marekebisho ya Bunge la Bajeti la Mwaka wa Fedha 2017/2018, zoezi hili la kuwatambua wafanyabiashara wadogo lilianza kutekelezwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kama vile Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) pamoja na Idara ya Uhamiaji”, alisema Kichere.
Kichere alieleza kwamba, TRA kwa kushirikiana na wadau hao, ilianza kutekeleza jukumu hilo kwa kuutambua Umoja wa Wamachinga wa Kariakoo jijini Dar es Salaam na kufanikiwa kuwapatia vitambulisho vya Taifa na Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) ambapo leo hii baadhi yao wamepatiwa vitambulisho maalum vya wafanyabiashara wadogo kama ishara ya uzinduzi wa utoaji wa vitambulisho hivyo.
Aliongeza kuwa, zoezi la kutambua vikundi mbalimbali vya wafanyabiashara wadogo na kuwapatia Kitambulisho cha Taifa na Namba ya Utambulisho wa Mlipa kodi linaendelea kufanyika nchi nzima na kubainisha kuwa, ili wafanyabiashara wadogo waweze kupata vitambulisho hivyo maalum, wanatakiwa kujiunga katika vikundi vinavyotambuliwa kisheria na Serikali, kuwa na Kitambulisho cha Taifa, kuwa na Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi ya kikundi alichojiunga nacho pamoja na kuchangia shilingi 10,000.
“Zoezi la kuwatambua wafanyabiashara wadogo linaendelea kufanyika nchi nzima na vitambulisho maalum vinavyotolewa kwa wafanyabiashara hao vitadumu na kutumika kwa kipindi cha miaka mitatu (3). Maelezo ya mfanyabishara mdogo yaliyopo kwenye kitambulisho hicho maalum ni pamoja na jina na picha ya mfanyabiashara, jina la eneo analofanyia biashara, Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi na Sahihi ya mfanyabiashara husika”, Alifafanua Kichere.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Ilala mkoani Dar es Salaam Mhe. Sophia Mjema aliishukuru Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe. Rais John Pombe Magufuli kwa kuwatambua wafanyabiashara wadogo ili waweze kupiga hatua kiuchumi kutoka daraja la chini hadi la kati na hatimaye kuweza kuchangia maendeleo ya nchi kupitia ulipaji wa kodi mbalimbali.
“Lakini kwanza naomba nimshukuru Mhe. Rais wetu John Pombe Magufuli kwa hii ndoto yake ya kuwasaidia wanyonge waliokuwa wanafanya biashara ndogo ndogo kutambulika na Serikali na kisha waondoke katika hali ya daraja la chini na kufikia daraja la kati. Nafurahi kuwaeleza kwamba, ndoto ya Mhe. Rais wetu imetimia”, alisema Mjema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Shirikisho la Wamachinga wa Kariakoo jijini Dar es Salaam Steven Lusinde alisema kuwa, wamefurahishwa na azma ya Serikali ya kuwatambua wafanyabiashara walio kwenye sekta isiyo rasmi kwa kuwa wamekuwa na hamu ya kuchangia maendeleo ya Taifa kwa muda mrefu.
“Sisi wamachinga tumekuwa na hamu kubwa sana ya kuchangia Taifa letu kwa sababu tunaamini chochote tunachokiona katika nchi hii bila sisi kuchangia hakiwezi kwenda”, alieleza Lusinde.
Moja ya majukumu ya Mamlaka ya Mapato Tanzania ni kukusanya mapato ya Serikali sambamba na kutoa elimu kwa walipakodi na watanzania kwa ujumla ili kuongeza uhiari wa ulipaji kodi na kuongeza mapato ya Serikali ambayo yanahitajika katika kuleta maendeleo ya nchi pamoja na wananchi wake.