Timu za watalaamu wa upimaji ardhi kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Tanzania na taasisi za usimamizi wa Ardhi nchini Kenya zimekutana wilayani Tarime mkoani Mara kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa kazi ya kuhakiki na kuimarisha mpaka wa Kimataifa baina ya nchi hizi mbili.
Mapema mwezi Machi, Naibu Waziri wa Adhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula alitangaza azma ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuanza kuimarisha mipaka yake kwa nchi jirani za Kenya na Uganda baada ya ziara yake ya kukagua mpaka wa Tanzania na Kenya katika Mbuga ya Wanyama ya Taifa ya Serengeti iliyopo mkoani Mara.
Hatua ya uhakiki na uimarishaji wa alama za mipaka ya mikataifa inatokana na mpaka huu kuwa wa siku nyingi na haukuwa wazi katika maeneo mengi pia baadhi ya alama hizo kuharibiwa, kung’olewa au kuchakaa na hivyo kusababisha Serikali pande zote kushindwa kusimamia kwa ufanisi shughuli za mipakani, rasilimali za nchi pamoja na ulinzi na usalama.
Katika uimarishaji wa alama hizo za mipaka hivi sasa, kutaongezwa alama mpya ndogo zinazoonana kwa umbali wa mita 100 pamoja na kubainisha eneo la ardhi huru kwa kila upande wa nchi (buffer zone).
Mpaka kati ya Tanzania na Kenya una jumla ya urefu wa Kilommita 760 kuelekea bahari ya Hindi ambapo awamu ya kwanza ya kazi ya uimarishaji mpaka inayofanyika hivi sasa itahusisha urefu wa Kilomita 238 kutoka kando ya Ziwa Victoria mkoani Mara hadi Ziwa Natron mkoani Arusha.
Baadaye, kazi ya uhakiki na uimarishaji wa mipaka itaendelea katika mikoa ya Kilimanjaro na Tanga na kisha itafanyika katika maeneo yote yanayohusika na mipaka ya kimataifa nchini.
Uimarishaji wa mipaka ya kimataifa nchini umefanyika mara ya mwisho mwaka 1975 kwa kurudishia alama ambazo ziliondolewa na kuongeza nyingine mpya kwa kuzingatia alama zilizopo.
Mbali na Kenya nchi nyingine zinazopakana na Tanzania ni; Msumbiji, Malawi, Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Burundi, Rwanda, Uganda pamoja na visiwa vya Komoro na Shelisheli.