Hatima ya vigogo sita wa Chadema wakiongozwa na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe kupata dhamana au kuendelea kusota gerezani itajulikana leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam ikiwa tayari wamekaa mahabusu saa 48.
Wengine ni katibu mkuu, Dk Vincent Mashinji; mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa; manaibu katibu wakuu, John Mnyika (Bara) na Salum Mwalimu (Zanzibar); na Mweka Hazina wa Baraza la Wanawake la chama hicho (Bawacha), Esther Matiko.
Viongozi hao wa juu wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini wanakabiliwa na mashtaka manane, likiwamo la kuhamasisha uasi, chuki na maandamano yaliyosababisha kifo cha mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini.
Wakati hatima ya viongozi hao ikisubiriwa, jana Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro iliwafutia mashtaka washtakiwa 44 kati ya 57 waliokuwa wakidaiwa kutenda makosa manane, likiwamo la kuchoma moto ofisi ya Serikali ya Kijiji cha Sofi wilayani Malinyi Novemba 26 mwaka jana.
Hakimu Ivan Msack wa mahakama hiyo aliwafutia mashtaka hayo baada ya upande wa mashtaka ukiongozwa na wakili wa Serikali, Sunday Hyera kudai hakuna ushahidi wa kutosha kuwatia hatiani.
Hata hivyo, washtakiwa wengine 13 wakiwamo wabunge Susan Kiwanga (Mlimba) na Peter Lijualikali (Kilombero) wataendelea na kesi hiyo na Aprili 24 itakuwa siku ya kusikilizwa maelezo ya awali.
Wakili wa washtakiwa hao, Fredy Kalonga alisema wanajiandaa kwa ushahidi utakaotolewa na upande wa mashtaka dhidi ya washtakiwa hao waliobaki.
Miongoni mwa waliofutiwa mashtaka ni diwani wa Mkula, Clemence Mjami aliyesema uamuzi wa Mahakama unaonyesha wazi namna upande wa mashtaka ulivyojikosoa kwa ushahidi dhaifu.
Kuhusu Mbowe na wenzake, juzi walisomewa mashtaka katika Mahakamani ya Hakimu Mkazi Kisutu na Wakili wa Serikali, Faraja Nchimbi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri katika kesi ya jinai namba 112 ya 2018. Wakili Nchimbi aliwasilisha pia ombi kwa Mahakama hiyo akitaka iwanyime dhamana washtakiwa akidai ni kwa sababu ya usalama wa umma wa Watanzania.
Hakimu Mashauri baada ya kusikiliza ombi hilo alisema atalitolea uamuzi leo. Katika makosa manane, mawili yanawakabili washtakiwa wote sita ambayo ni kufanya mkusanyiko au maandamano yasiyo halali Februari 16 wakidaiwa kufanya hivyo wakiwa Barabara ya Kawawa, Kinondoni Mkwajuni.
Shtaka la pili, viongozi hao wa Chadema wanadaiwa wakiwa na watu wengine 12 ambao hawajafikishwa mahakamani, waligoma kutii amri ya kusambaratika na kuvunja mkusanyiko huo uliosababisha kifo cha Akwilina huku maofisa wa polisi wakipata majeraha. Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni anadaiwa kuhamasisha chuki kwa wanajamii isivyo halali na ushawishi wa utendekaji wa kosa la jinai. Mchungaji Msigwa anashtakiwa akidaiwa kushawishi raia kutenda kosa la jinai.