SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Alhamisi, 29 Machi 2018

T media news

Licha ya Times FM Kuomba Radhi TCRA Yawakalia Kooni Yasema Kibano Kipo Palepale

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imesema licha ya kituo cha Redio Times kuomba radhi katika kipindi cha mahojiano kati yake na msanii Diamond, hatua ya kufika mbele ya kamati ya maudhui kwa ajili ya kuhojiwa ipo pale pale.

Hayo yamesemwa leo Machi 29 na Ofisa Mkuu Idara ya Utangazaji wa mamlaka hiyo, Andrew Kisaka, alipohojiwa na MCL Digital, na kutakiwa kueleza kama uombaji wa radhi  wa kituo hicho ndio salama yao ya kutoitwa mbele ya kamati hiyo kujieleza kwa nini wasichukuliwe hatua.

Katika maelezo yake, Kisaka amefafanua kwamba suala la kituo cha Redio au Televisheni kinapokosea ni lazima uongozi wake ufike mbele ya kamati hiyo na kuongeza kuwa hiyo ni sheria hivyo huwezi kuikwepa.

Amesema sheria hiyo inabaki palepale hata kama itatokea uongozi huo, ukaomba radhi kwa kupitia njia nyingine kama hiyo waliyoifanya times.

Sakata la Diamond, Times FM waomba radhi

Akielezea kuhusu adhabu inayotolewa kwa kituo ambacho kimekosea, amesema ni pamoja na kupigwa faini au kufungiwa na hii inategemea na uzito wa kosa na kuangaliwa kama makosa ya aina hiyo yamekuwa yakijirudia mara kwa mara.

Jana katika taarifa yao, Kituo hicho cha Redio Times cha jijini Dar es Salaam kilichorusha mahojiano ya  mwanamuziki huyo anayefanya vizuri kwenye muziki wa Bongofleva, kiliomba radhi kwa kauli tata zilizozua mjadala nchini.

Taarifa hiyo iliyowekwa jioni katika mtandao wa kijamii wa Instagram, ilisema Times, imeamua kuomba radhi kutokana na kauli tata alizotumia msanii huyo wakati akihojiwa katika kipindi cha Play List kinachoongozwa na mtangazaji Omary Tambwe.

“Kwa namna ambayo haikutarajiwa , mwanamuziki huyo alitumia kauli  tata dhidi ya Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni , Sanaa na Michezo, Juliana Shonza katika mahojiano hayo.

Taarifa ya Times ya kuomba radhi imesema: “Uongozi wa Times unaomba radhi kwa Wizara, Naibu Waziri, TCRA, Basata pamoja na umma kutokana na kauli hiyo ya Diamond kwani Times haikuwa dhamira yetu kwa sintofahamu hiyo na tumekuwa tunafanya jazi kwa kuzingatia sheria na taratibu za utangazaji.”