SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumanne, 18 Aprili 2017

T media news

CAG: Mkataba wa Mlimani City na Chuo Kikuu cha UDSM ni Wizi Mtupu..!!!


RIPOTI ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), imeanika madudu ya mkataba wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kwenye mradi wa Mlimani City.

Madudu hayo yanaonyesha namna chuo hicho kinavyopoteza mamilioni ambako amependekeza mkataba huo ufanyiwe marekebisho.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyowasilishwa bungeni hivi karibuni, ujenzi wa mradi wa Mlimani City ulianza Oktoba Mosi mwaka 2004, ukikadiriwa kukamilika Septemba Mosi mwaka 2016.

Hata hivyo, CAG ameshauri yafanyike marekebisho katika baadhi ya vifungu vya mkataba huo.

Ripoti hiyo inaonyesha kwamba moja ya sababu ya kukiukwa maeneo ya mkataba wa wabia hao wawili ni uzembe wa menejimenti ya chuo.

Ripoti inasema: “Tulibaini kwamba mradi mdogo wa hoteli ya nyota tatu (ambayo ina vyumba 100 kikiwemo chumba cha mikutano kinachochukua watu 1,000) na uboreshaji wa bustani ya botania, ikiwa ni sehemu ya mradi wa Mlimani City, haujakamilika kwa kipindi cha miaka 10 tangu tarehe ya makubaliano ya kumaliza mradi.

“Mtazamo wangu ni kuwa hakuna ufuatiliaji wa karibu, usimamizi na tathmini ya mkataba huo kwa uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

“Kwa sababu hiyo kuna uwezekano wa kushidwa kumalizia kazi iliyobaki kwa sababu ya ongezeko kubwa ya gharama ya kumalizia mradi tangu kipindi kilichopangwa kupita.

“Menejimenti ya Chuo Kikuu inashauriwa kuuangalia upya mkataba iliouingia na Mlimani City Holding, kuharakisha umaliziaji wa miradi,” ilieleza ripoti hiyo ya CAG.

Ripoti hiyo pia inaainisha ukiukwaji wa ulipaji wa ada ambayo mwekezaji anatakiwa kuitoa kwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa kifungu cha 1.1(j) cha mkataba pamoja na kifungu 10.1 cha hati ya ukodishaji wa uwanja, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kinapaswa kipate asilimia 10 ya mapato ya kodi ghafi.

“Kinyume na kufungu tajwa hapo juu, Mlimani Holding Limited (MHL), hufanya hesabu za gawio la kodi ya Chuo Kikuu kwa kuzingatia asilimia 10 ya mapato ya kodi baada ya kutoa gharama za uendeshaji badala ya kujumuisha gharama za uendeshaji.

“Ukiukwaji huu unakifanya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuwa katika hatari ya kupoteza kiasi kikubwa cha mapato kutoka katika mradi wa Mlimani City,” inasema ripoti hiyo.

CAG anaishauri menejimenti ya chuo hicho ifanye upya hesabu za gawio lake la asilimia 10 kutokana na mkataba na kuomba kulipwa na mpangaji kiasi kilichokuwa kimekosewa.

Pia alishauri kuwasiliana na mpangaji na kufikiria kubadilisha mkataba kuweka vifungu ambavyo vitaruhusu idara ya ukaguzi ya ndani ya chuo kuangalia mapato na gharama za uendeshaji za mradi.

Ripoti hiyo pia imeainisha udhaifu wa ufuatiliaji na usimamizi wa mapato kutoka kwa wapangaji wadogo kwenye mradi huo.

Inasema kifungu cha 11.2(l) cha hati ya makubaliano, mpangaji (MHL) anapaswa kutopangisha mtu yeyote ambaye hajathibitishwa na Mpangishaji (Chuu Kikuu cha Dar es Salaam), ikiwa ni njia ya kudhibiti mapato yake.

Kinyume na makubaliano ya hayo, ukaguzi wa CAG umebaini kwamba MHL amepangisha majengo kwa wapangaji wengine bila kupata kibali cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

“Kuna upungufu wa utekelezaji wa vipengele vya mkataba kwa upande wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam hivyo kusababisha Chuo kushindwa kujua kwa usahihi mapato ya kodi kutoka kwa wapangaji wote.

“Menejimenti ya Chuo Kikuu cha Dar-es-salaam inashauriwa kutekeleza vifungu na vipengele vyote vya hati ya makubalian ya upangaji kikiwamo kifungu 11.2 (l) cha hati ya makubaliano ambacho kinakitaka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuwathibitisha wapangaji wadogo wadogo,” anashauri CAG.

Ripoti hiyo pia inaonyesha mapitio ya mkataba wa upangishaji wa ardhi kati ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Mlimani Holding Limited yamegundua kwamba mkataba haumpi mmiliki wa ardhi haki ya kukagua kazi zinazofanywa na mpangaji.

“Katika hali hii, mpangishaji, ambaye ni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam hawezi kujua endapo mpangaji, Mlimani Holding Limited, anakiuka mkataba katika uendeshaji au kuna baadhi ya wapangaji wa nyumba hawawekwi wazi na mpangaji huyu,” inasema ripoti.

CAG anashauri Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuwasiliana na Mlimani Holding Limited kupata haki ya kukagua shughuli za miradi kwa manufaa ya pande zote mbili.

Ripoti hiyo inasema pia kwamba mapitio ya mkataba yamegundua mkataba huo hauelezei hali halisi ya ugawanaji mali mkataba utakapoisha (miaka 50 au 85 kutokana na makubaliano ya pande mbili).

“Hakuna makubaliano yoyote yanayoelezea mgawanyo wa mali na miondombinu itakayokuwapo wakati mkataba unaisha.

“Kwa hali hii, kuna uwezekano wa kutokea mvutano wa sheria mwisho wa mkataba. Hali hii ikitokea, Chuo Kikuu kitakosa msaada wa sheria.

“Uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, unashauriwa kuingia katika mazungumzo na Mlimani Holding Limited kuweka vifungu vitakavyoonyesha haki ya kila upande wakati wa mkataba utakapoisha,” anaeleza CAG.

Ripoti hiyo pia inasema Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ( kiliingia katika makubaliano na kampuni ya Ernest and Young kufanya ukaguzi maalumu kujua kiasi cha mapato ambacho kinaidai kampuni ya Mlimani Holding Limited katika kipindi cha Mei Mosi mwaka 2006 mpaka Juni 30 mwaka 2014 na kubaini kutolipwa dola za Marekani 57,607.

“Wakati wa ukaguzi niligundua kuwa kiasi cha Dola za Marekani 309,458 kilitakiwa kipokelewe na Chuo kutoka MHL, lakini usuluhisho wa hesabu ulionyesha MHL ililipa Dola za Marekani 213,850 kupitia uhamisho wa benki kwa njia ya eletroniki na kubakisha Dola za Marekani 57,607.

“Kuna ufuatiliaji duni kwa upande wa menejimenti ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika kukusanya deni hilo. Menejimenti ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam inashauriwa kuongeza nguvu katika kufuatilia na kukusanya deni wanalolidai MHL,” inasema ripoti hiyo.