Mwanasiasa wa upinzani Kenya aliyeidhinisha kiapo cha kiongozi wa upinzani Raila Odinga kuwa 'Rais wa Wananchi' Januari Miguna Miguna ametimuliwa tena kutoka nchini humo.
Mwanasiasa huyo ametimuliwa huku mzozo kuhusu uraia wake ukiendelea.
Bw Miguna ameandika kwenye Facebook kwamba ameamka na kujipata yuko Dubai na kwamba anahitaji matibabu.
Amesema anafahamu kwamba kuna mpango wa kumpeleka London lakini anataka kupanda ndege ya kurejea Nairobi pekee.
Mwanasiasa huyo amesema amesindikizwa na afisa wa idara ya ujasusi.
Serikali imechukua hatua hiyo licha ya kuwepo kwa maagizo ya mahakama ya kuzuia kutimuliwa kwake na ya kuitaka serikali kufanikisha kurejea kwake nchini humo.
Mawakili wa Bw Miguna wamethibitisha kwamba aliondolewa nchini humo kwa kutumia ndege ya shirika la Emirates iliyokuwa inaelekea Dubai.
Bw Miguna alikuwa amezuiliwa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) tangu alipowasili Jumatatu adhuhuri.
Mwanasiasa huyo alikuwa anajaribu kurejea kutoka Canada ambako alikuwa amepelekwa baada ya kufurushwa kutoka Kenya kwa lazima mwezi Februari.
Jaji wa Mahakama Kuu George Odunga Jumatano alisema waziri wa usalama nchini humo, mkuu wa polisi na mkuu wa idara ya uhamiaji watakuwa wamekaidi maagizo ya mahakama iwapo wangekataa kumwachilia huru.
Alikuwa ametoa ilani kwa watatu hao kufika mahakamani baadaye Jumatano lakini baada yao kukosa kufika akawapata na hatia ya kukaidi agizo la mahakama.
Aliahidi kutoa adhabu dhidi yao leo asubuhi.
Maafisa wa Kenya mnamo 6 Febuari walikuwa wamemfukuza kutoka nchini humo kutokana na mchango wake wakati wa kuapishwa kwa Bw Odinga.
Walisema mwanasiasa huyo hana uraia wa Kenya lakini ana uraia wa Canada.
Idara ya uhamiaji ya Kenya imekariri kuwa Miguna alipoteza uraia wa Kenya mwaka 1998 alipopewa uraia wa Canada wakati ilipokuwa ni kinyume cha sheria kuwa na uraia wa nchi mbili nchini Kenya
Kuzuiliwa kwa Bw Miguna kumejadiliwa pakubwa kwenye mitandao ya kijamii Kenya, baadhi wakiunga mkono hatua hiyo lakini wengine wakiwashutumu maafisa wa uwanja wa ndege na serikali.
Mmoja wa mawakili wa Bw Miguna, Nelson Havi, ni miongoni mwa waliokuwa wa kwanza kufichua kwamba Bw Miguna alikuwa ametimuliwa tena nje ya nchi hiyo