Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Taifa UVCCM, Kheri James amewataka vijana wa umoja huo kuwa tayari kulinda heshima ya nchi kwa gharama yeyote dhidi ya vibaraka ambao wanataka kuchafua taswira ya nchi kwa lengo la kuwanufaisha mabeberu.
Kheri ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na vijana wa umoja huo mjini Dodoma na kusema lengo la kufanya hivyo ni kutokana na kuwepo na matumaini makubwa ya kiuchumi yaliyorejeshwa na serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli hivyo hawapo tayari kuona kikundi cha watu wachache wanaotaka kuwarudisha nyuma kimaendeleo.
"Kuanzia sasa endapo akiibuka mtu mwenye ujasiri wa kutukana, vijana hawatotukana bali watafanya litakaloonekana linafaa kwa maslahi ya taifa kwani wapo wanaojipambanua wazi kusifu viongozi wa ulimwengu mzima lakini kamwe hawawezi kuwapongeza na kuwasifu kwa chochote viongozi wa nchi", amesema Kheri James.
Naye Kaimu Katibu UVCCM, Shaka Hamdu Shaka amesema serikali imeona uwepo wa vijana makao makuu na kuthamani uwepo wao kutokana na kuendesha mambo kisasa zaidi.
Kwa upande wake mbunge wa viti maalum vijana, Mariam Mzuzuri amesema maamuzi na tamko la mwenyekiti wa uvccm taifa watalifanyia kazi ili vijana waweze kutambua fursa walizonazo hususania mkoani Dodoma ambako hivi sasa ni makao makuu ya nchi.