Kikosi cha Taifa Stars kimeibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo katika mchezo wa kirafiki uliochezwa Uwanja wa Taifa jioni ya leo.
Mechi hiyo ya kalenda ya FIFA ilikuwa na mashambulizi ya zamu kwa timu zote mbili haswa katika kipindi cha kwanza kilichotawaliwa zaidi na wenyeji Stars.
Stars ilianza kuandika bao la kwanza katika dakika ya 74 kupitia kwa Mshambuliaji anayekipiga KRC Genk ya Ubelgiji, Mbwana Samatta, kufuatia kazi nzuri ya Shiza Kichuya aliyepiga krosi safi kushoto mwa Uwaja na kumkuta Samatta ambaye bila ajizi akapiga mpira kwa Kichwa.
Dakika ya 86, Shiza Kichuya alioongezea Taifa Stars bao la pili kwa shuti kali la mguu wa kushoto, baada ya kutengenezewa pasi murua na Mbwana Samatta.
Mpaka dakika 90 zinamalizika, Stars 2, Congo 0.
Ushindi huo unarejesha furaha na matumaini kwa Watanzania, baada ya kupoteza mchezo uliopita dhidi ya Algeria kwa jumla ya mabao 4-1 ugenini.