SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumanne, 27 Machi 2018

T media news

Waziri Jafo Atekeleza Agizo la Rais Magufuli la Kuwasimamisha Kazi Wakurugenzi Wawili

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa  Selemani Jafo  amewasimamisha kazi wakurugenzi wawili kati ya watatu wa Halmashauri za Pangani na Kigoma baada ya kupata hati chafu katika matokeo ya Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka 2016/17.

Ripoti hiyo iliyowasilishwa leo Machi 27, 2018 inaonyesha halmashauri 166  kupata hati safi, 16 hati zenye shaka na halmashauri tatu kupata hati chafu.

Umauzi huo unafanyika ikiwa ni dakika chache baada ya Rais John Magufuli kutoa agizo hilo.

Halmashauri zilizopata hati chafu ni Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji na Halmashauri ya Kigoma na Pangani.

Waziri Jafo amesema baada ya kuwasimamisha,  amemwagiza katibu mkuu wa wizara hiyo kuunda timu ya watalaamu kuchunguza hati hizo na kutoa matokeo ndani ya wiki tatu.

Amesema wakurugenzi waliohusika katika hati chafu ni Daud Mlahagwa (Pangani), aliyekuwa Mkurugenzi wa Kigoma Ujiji, Judethadeus Mboya ambaye amestaafu kwa sasa.

“Amestaafu lakini ameacha mambo yakiwa hayako sawa, wakati akiwa ‘account officer’ mambo yalikwenda kombo na halmashauri hiyo ilipata hati chafu kwa miaka mitatu mfululizo,” amesema.

Mwingine ni Mkurugenzi wa halmashauri ya Kigoma, Hanji Godigodi na Damian Chambasi wa Pangani.

“Wakurugenzi hawa waliosababisha hati chafu nawasimamisha kazi kuanzia leo Machi 27, 2018 hadi hapo uchunguzi wa utendaji wao utakapokamilika, hawa wawili nawasimamisha kazi, kutokana na hili namwagiza katibu Mkuu wa Tamisemi kuunda timu ya watalaamu kwenda kuchunguza utendaji kazi wa wakurugenzi hao na kunipatia taarifa ndani ya wiki tatu,”amesema.

Amesema taarifa itakayopatikana itabainisha kiwango cha uchafu huo na Serikali itachukua hatua nyingine za kisheria kadri uchunguzi utakavyoelekeza.

Pia, amewataka wakurugenzi katika halmashauri zilizofanya vizuri katika ukaguzi huo, waendelee kutekeleza na majukumu yao na kutoa majibu ya hoja zote zilizobainishwa na ripoti ya CAG.

Amesema Serikali imeanza kufanya vizuri katika ukaguzi huo baada ya kufikia asilimia 90 na matumaini yaliyopo ni kuondokana na taarifa ya hati chafu ili kuhakikisha fedha za Serikali zinatumika kwa maendeleo ya wananchi.