IKIWA ni saa 48 zimepita tangu Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na viongozi wenzake watano wa chama hicho kupelekwa katika mahabusu ya Segerea baada ya kunyimwa dhamana katika kesi yao waliyosomewa juzi Machi 27, Katika Mahakama ya Kisutu Dar, wafuasi wa chama hicho waliofurika mahakamani hapo wamezua sintofahamu baada ya kufanya vurugu wakipiga makelele na kuimba wakitaka haki.
Wafuasi hao waliokuwa nje ya geti la mahakama hiyo wakiwa wamekusanyika baada ya Jeshi la Polisi kuwazuia kuingia mahakamani kusikiliza kesi ya viongozi hao walianza kupiga makelele wakiimba ‘hatupoi hatupoi, tunataka haki tunataka haki’, hali iliyowalazimu polisi kutia kambi eneo hilo na kuimarisha ulinzi kuhakikisha hakuna uvunjifu wowote wa amani unafanyika.
Kesi hiyo ilitarajiwa kuendelea tena leo Machi 29, ili kufanya jitihada za kupata dhamani. Viongozi wengine waandamizi wa Chadema wanaoshtakiwa katika kesi hiyo ni: Vicent Mashinji, John Mnyika, Peter Msigwa, Ester Matiko na Salum Mwalimu, watapandishwa mahakamani kwa ajili ya kusomewa masharti ya dhamana kama ipo au haipo.