Mwenyekiti wa Chama cha TLP, Augustine Mrema amesema yeye ni miongoni kwa watu ambao wamekuwa wakifuatilia muziki wa wasanii wa hapa nchini na kati ya watu ambao wanamkuna ni Naseeb Abdul maarufu kama Diamond.
Mrema amesema kwamba anapenda sana nyimbo za mwanamuzi huyo na kwa muda mrefu amekuwa akizifuatilia.
“Nampenda sana Diamond si ndiyo yule aliyeimba ‘zilipendwa huku akitutaja mimi na Lipumba? Huyu mtoto anajua kuimba,”anasisitiza.
Mrema amesema kuwa wimbo huo ametokea kuupenda kwa kwa sababu unaonyesha hali halisi ya maisha yake sasa kwa kuwa ni ukweli usiopingika kwamba yeye na Lipumba sasa ni zilipendwa.
“Kweli tumekuwa wazeee, wakati wetu umefika na sasa tunatakiwa kuwapisha vijana waendeleze gurudumu lakini usifikirie mimi mzee ukajua sisikilizi muziki wa kizazi kipya nasikiliza zote na ninafurahi sana wanafanya kazi nzuri,”ameongeza.