Mchungaji mmoja nchini Msumbiji amejikuta akiishia mikononi mwa polisi baada ya kujaribu kumfufua mwanamume mmoja eneo la kati la Msumbiji bila mafanikio.
Mchungaji huyo alidai kuwa roho mtakatifu alimwambia asafiri hadi katika hospitali inayofahamika kwa jina Chimoio iliyopo katika jimbo la Manica, ili akafanye muujiza ambao alidai ana uwezo wa kufanya na alipowashawishi Maafisa wa hospitali walimruhusu aingie ndani ya chumba cha kuhifadhi maiti ili atekeleze muujiza huo.
Hata hivyo baada ya siku mbili za maombi, hakuweza kurejesha uhai wa marehemu na familia hiyo haikushangazwa na kushindwa kwake.
Dada wa marehemu ambaye hakutaka jina lake litajwe aliwaambia waandishi wa habari kuwa “Kasisi aliomba, akaomba na kuomba hadi akanena kwa lugha. Alizungusha kichwa cha marehemu huku na kule huku akiomba.
“Lakini hakuna hata sehemu ya marehemu kaka yangu iliyoweza kutikisika. Wakati mmoja kasisi alipaza sauti akisema, ‘amka, kijana wa Mungu!, Hatukuamini angefanya mwujiza wowote. Hii ni kwa sababu hakuwahi, hata wakati mmoja, kuthibitisha uwezo wake wa kumrejeshea mfu uhai wake.
“Tangu wakati huo kasisi alikamatwa na yuko mikononi mwa polisi akishtakiwa kwa kosa la kumkosea heshima mfu."Alisema Dada wa Marehemu