Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Aprili 24 na 25, 2018 itaanza kusikiliza ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka katika kesi inayomkabili Mkurugenzi Mkuu wa zamani wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Tido Mhando.
Tido anakabiliwa na mashtaka manne ya kutumia madaraka vibaya na moja la kuisababishia Serikali hasara ya Sh887.1 milioni.
Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai leo Machi 28, ameieleza kwa Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi kuwa kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kusikilizwa kwa ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka.
Ameieleza kuwa kesi hiyo ilikuwa inasikilizwa na Hakimu Victoria Nongwa ila kwa sasa imepangwa kusikilizwa mbele yake.
Baada ya kutolewa kwa maelezo hayo, Hakimu Shaidi ameipanga kuisikiliza kesi hiyo Aprili 24 na 25, 2018 ambapo upande wa mashtaka umedai utaita mashahidi wawili Aprili 24 na mashahidi wengine wawili Aprili 25,2018.
Inadaiwa kuwa Juni 16, 2008 akiwa Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Tido ambaye alikuwa mkurugenzi wa TBC, kwa makusudi alitumia madaraka yake vibaya kwa kusaini mkataba wa kuendesha na utangazaji wa vipindi vya televisheni kati ya TBC na Channel 2 Group Corporation (BV1) bila ya kupitisha zabuni jambo ambalo ni kinyume na Sheria ya Manunuzi ya Umma na kuinufaisha BVl.
Katika shtaka la pili, Tido anadaiwa kutumia vibaya madaraka yake Juni 20, 2008 aliposaini makubaliano kwa utangazaji wa dijitali duniani kati ya TBC na BVl.
Katika shtaka la tatu, anadaiwa Agosti 11, 2008 na Septemba 2008 akiwa Dubai, Tido alitumia vibaya madaraka yake kusaini mkataba wa makubaliano kwa ununuzi, usambazaji kufunga vifaa vya usambazaji na mnara wa utangazaji kati ya TBC na BVI na kuifaidisha BVI.
Katika shtaka la nne, anadaiwa kuwa Novemba 16, 2008 akiwa Dubai, Tido alitumia vibaya madaraka yake kusaini mkataba wa makubaliano kwa kuendesha miundombinu ya utangazaji (DTT Broadcast Infrastructure) kati ya TBC na BVI na kuinufaisha BVI.
Katika shtaka la mwisho, anadaiwa kuwa kati ya Juni 16 na Novemba 16, 2008 akiwa UAE, Tido aliisababishia TBC hasara ya Sh887.1 milioni.
Tido anatetewa na Wakili Ramadhani Maleta na yupo nje kwa dhamana.