SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatano, 28 Machi 2018

T media news

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Madawa Afunguka Alivyokataa Rushwa ya Milioni 800


MAMLAKA ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya imemtia mbaroni mfanyabishara wa kemikali bashirifu, mkazi wa Mwanza ambaye alitaka kuwahonga mamilioni ya fedha makamishna wa mamlaka hiyo ili wavuruge kesi inayomkabili.

Mfanyabiashara huyo ambaye jina lake halikutajwa kutokana sababu za usalama, inasemekana baada ya kukamatwa, aliahidi kumhonga Sh milioni 800  Kamishna Mkuu wa Mamlaka hiyo, Rogers Siang’a   amsaidie kufuta shitaka lake.

Pia, mtuhumiwa huyo aliahidi kumpa rushwa ya Sh milioni 400  Kamishna wa Sheria wa Mamlaka hiyo, Edwin Kakolaki ili naye amsaidie kuvuruga kesi iliyokuwa ikimkabili.

Siang’a alikuwa akizungumza juzi mjini hapa wakati wa semina ya Kamati ya Kudumu ya Bunge inayoshughulikia Ukimwi na Dawa za Kulevya.

Alisema viwango vikubwa vya kemikali bashirifu ambayo mara nyingine hutumika kutengenezea dawa za kulevya,  imekuwa  ikiingizwa nchini.

“Kuna zaidi ya kampuni 2000 zimekuwa zikiingiza kemikali bashirifu nchini  lakini kasi ya kuzikagua kemikali hizo imekuwa ndogo kutokana na wingi wa kampuni na uchache wa rasilimali watu na fedha.

“Lakini  Desemba mwaka jana, kuna mfanyabiashara mmoja wa kemikali bashirifu alitaka kumpa hongo Kamishna Kakolaki, ya Sh milioni 400  avuruge kesi, ila kwangu alisema akinifikia  atanipa Sh milioni 800,” alisema   Siang’a.

Kamishna wa Kinga na Tiba kwenye mamkala hiyo, Dk. Peter Mfisi, alisema hadi sasa   Watanzania 1050 wamekamatwa katika nchi mbalimbali wakituhumiwa kuhusika na biashara ya dawa za kulevya.

Alisema kitendo hicho kimekuwa kikichafua hadhi ya Tanzania katika sura ya  mataifa.

“Hata hivyo, udhibiti wetu umefanikiwa kudhibiti uingizwaji wa dawa hizo nchini na kusababisha kuongezeka kwa watu wanaohitaji matibabu ya ‘methadone   na kupanda kwa bei ya dawa hizo mtaani.

“Kwa ujumla, hali bado ni mbaya kwa watumiaji wa dawa hizo hasa kutokana na kuambukizana magonjwa ya Ukimwi, TB na homa ya ini kwa sababu watumiaji hao  wana tabia ya kuchangia sindano.

“Lakini mtumiaji akimuona mwenzake anasinzia wakati akiwa amejichoma sindano, basi hunyonya damu ya mwenzake kwa kutumia sindano kisha kujidunga akiamini kuwa damu ya mtu huyo ina dawa za kulevya,” alisema.

Waziri wa Nchi, Sera, Uratibu, Bunge, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, alisema kutokana na udhibiti wa dawa hizo kuimarika, wafanyabiashara wameanza kuwatumia watoto wa viongozi na matajiri wakiamini wana uwezo wa kununua dawa kwa urahisi.

“Pamoja na hayo, Serikali itawasaka kila kona bila kujali mtu au nafasi aliyonayo   kuhakikisha mtandao huo unatokomea,” alisema.

Naye Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya Bunge, Oscar Mukasa, alisema lengo la semina hiyo ni kuwapa mwanga wajumbe wapya wa kamati hiyo  wafahamu utendaji kazi na muundo wa mamlaka hiyo.

Pamoja na hayo, alisema kamati yake itashirikiana na mamlaka husika na Serikali ili vita dhidi ya dawa za kulevya, ifanikiwe.