SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Alhamisi, 28 Aprili 2016

T media news

Serikali Kuendelea Kuwachukulia Hatua Waliobadili Matumizi ya Ardhi Ya Makazi kuwa ya Biashara


Serikali imesema kuwa itawachukulia hatua za kisheria wananchi waliobadili matumizi ya Ardhi ya makazi kuwa maeneo ya biashara kinyume cha sheria na kuifanya Serikali kukosa mapato  stahiki ya kodi ya Ardhi.

Hayo yamebainishwa  leo jijini Dar es salaam na Kaimu Mkuu wa Kitengo Cha Kodi toka Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi  Bi.Rehema  Kilonzi wakati  akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu  mapato yaliyokusanywa kutokana na kodi ya pango la ardhi kwa mwaka  fedha 2015/2016.

Amesema kuwa  baadhi ya wananchi katika maeneo mbalimbali nchini wameyageuza maeneo yaliyopangwa kwa ajili ya makazi ya watu kuwa maeneo ya nyumba za kulala wageni,hosteli, maeneo ya biashara jambo ambalo ni kinyume cha Sheria ya Ardhi Namba 4 ya mwaka 1999 chini ya fungu la 33.

“Rai yetu kwa wananchi waliopata fursa ya kumiliki maeneo yaliyopangwa na kumilikishwa kisheria,tunawaomba walipe kodi ya Pango la ardhi kwa wakati kuepuka usumbufu wa kufikishwa Mahakamani .”alisisitiza  Kilonzi.

Amesema katika kipindi cha mwaka wa 2015/2016 Serikali imefanikiwa kukusanya kiasi cha Bilioni 60 kutokana na kodi ya Pango la Ardhi ambazo ni sawa na asilimia 85 ya lengo lililowekwa la kukusanya shilingi bilioni 70.

Amesema  mkakati wa wizara  hiyo ni kuhakikisha kuwa inafikia lengo la kukusanya Kodi  hiyo na kuongeza kuwa hiyo imesambaza maafisa wake katika Ofisi zote za Kanda ili kuhakikisha kuwa Halmashauri na Manispaa zinasambaza hati za madai ya Kodi ya pango la Ardhi na kuwafikia wadaiwa wote kwa wakati muafaka.

Amesema wizara hiyo inaendelea na mkakati wa kufungua mashauri ili kupata kibali cha mahakama cha kukamata mali za wadaiwa sugu na  kuwapokonya hati milki katika maeneo mbalimbali nchini.

Akizungumzia hatua hiyo amesema kuwa katika  jiji la Dar es salaam mashauri yataanza kusikilizwa katika Baraza ya Nyumba na Ardhi La Wilaya ya Kinondoni kuanzia mwezi Mei 2016,  kisha zoezi hilo litaendelea kwa Mikoa na Wilaya zote Jijini hilo.

Akitoa ufafanuzi kuhusu Kodi ya Ardhi inayotozwa na wizara hiyo amesema kuwa  inatozwa kwa kuzingatia Sheria ya Ardhi Namba 4 ya mwaka 1999 chini ya fungu la 33.

Amesema kuwa katika kipindi cha mwezi mmoja na nusu ( kuanzia Februari 2016) Wizara imewafikia  wamiliki wa Ardhi 679 katika Maeneo ya Sinza na Kijitonyama Jijini Dar es salaam na kufanya uthamini wa maendelezo kwa kwa wale waliokiuka masharti ya matumizi yaliyopangwa ambapo ilibainika kuwa kuna ukiukwaji wa masharti ya Uendelezaji kwa kubadili matumizi yaliyoainishwa katika milki zao.

Aidha, amesema kutokana na uthamini uliofanyika mwezi Februari Serikali inatarajia kukusanya jumla ya milioni mia nane kama faini kutokana na ubadilishaji wa matumizi ya maeneo usiozingatia Sheria za Ardhi katika maeneo ya Sinza na Kijitonyama.