SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Ijumaa, 29 Aprili 2016

T media news

 ‘ANAYEWACHEZESHA KAGERA SUGAR NJE YA KAITABA KWA MIEZI 18 SASA NDIYE WA KULAUMIWA WAKISHUKA’

Na Baraka Mbolembole

Kitendo cha kukubali kufungwa 2-0 na Ndanda SC katika mchezo wao wa 27 ni pigo kubwa ambalo naliona na si ajabu Kagera Sugar ikashuka daraja katika namna isivyotarajiwa na ye yote. Misimu kumi mfululizo yenye kupanda na kushuka kwa timu hiyo ya Misenyi ilijijenga na kuonekana timu yenye uwezo kumaliza nafasi nne hadi 6 za juu katika ligi kuu ya Tanzania.

Baada ya timu hiyo kuchukuliwa na kiwanda cha uzalishaji sukari (Kagera Sugar) mwanzoni mwa miaka ya 2000 kutoka kwa wananchi (awali timu hii ilikuwa ikifahamika kama Kagera Stars.) Chini ya mkufunzi marehemu, Slivester Marsh (Mwenyezi Mungu amrehemu) timu hiyo ikafanikiwa kupanda daraja hadi ligi kuu mwaka 2005.

Ikashinda taji la michuano iliyopotea ya Tusker Cup mwaka 2007 ikiwa na wachezaji wengi vijana kama Amri Kiemba, Vicent Barnabas na baadhi ya wazoefu kama Yusuph Macho. Omar Changa na Karume Songoro. Kagera ni timu inayowavutia wapenzi wengi wa kandanda nchini kutokana na kuzishinda timu kubwa za Yanga na Simba mara kwa mara katika uwanja wake wa nyumbani.

Misimu mitatu iliyopita waliweza kumaliza katika nafasi ya nne na misimu yao miwili ya mwisho wamemudu kubaki miongoni mwa timu 6 za juu katika VPL.

KUCHEZA UGENINI

Kikawaida kila timu ina jivunia kucheza mechi zake katika uwanja wa nyumbani mbele ya mashabiki wao. Mashabiki huchangia kuhamasisha wachezaji wao wawapo uwanjani na uwepo wake umuongezea morali zaidi mchezaji na kuhitaji kufanya vizuri ili kumridhisha shabiki wake.

Masikini, Kwa miezi karibia 18 sasa timu hii inatangatanga huku na huko, mara CCM Kirumba, Mwanza, mara Kambarage, Shinyanga mara Ally Hassan Mwinyi, Tabora huko kote kuweka makazi na kuvitumia viwanja hivyo kama uwanja wao wa nyumbani.

Kaitaba Stadium, Bukoba ndiyo uwanja wa nyumbani wa Kagera Sugar lakini tangu ulipoanza kufanyiwa ukarabati ikiwemo kubadilisha kwa sehemu ya kuchezea kwa uwekwaji wa nyasi bandia kabla ya kuanza kwa mzunguko wa pili msimu uliopita (2014/15) hadi sasa timu hiyo imekuwa ikicheza ugenini.

Kwasasa timu hiyo ipo chini ya mwalimu mzoefu Adolf Richard ambaye amefanikiwa kuisaidia kushinda michezo 6 kati 22 aliyoisimamia timu hiyo hadi sasa. Kagera wako nafasi ya 12 wakiwa na alama 25 (pointi tatu zaidi ya Coastal Union inayoshika mkia, pointi mbili zaidi ya African Sports iliyo nafasi ya 15, pointi mbili zaidi ya JKT Mgambo iliyo nafasi ya 14 kwa timu zitakazoshuka, pointi moja zaidi ya JKT Ruvu yenye michezo miwili zaidi ya viporo.)

Kagera, Mgambo, Sports na Coastal zote zimecheza game 27. Kagera watacheza na Stand kisha Azam na kukamilisha msimu kwa kuwavaa Mwadui FC. Pointi 9 zilizo mbele yao kama watazipata zitawafanya kufikisha alama 31. Ni Toto Africans na Mbeya City pekee ndio bado hazina uhakika wa kusalia lakini timu hizo tayari zimekusanya alama 30.

Huu ni wakati wa timu za Kagera, JKT Ruvu, Mgambo, Sports na Coastal kuombeana njaa kwani timu 3 za kwenda ligi daraja la kwanza zitatoka katika kundi lao. Anayewafanya Kagera Sugar wacheze nje ya Kaitaba kwa miezi 18 sasa ndiye atapaswa kulaumiwa ikiwa timu hii itashuka daraja baada ya misimu kumi mfululizo kwenye ligi.

‘Anayewachezesha Kagera Sugar nje ya Kaitaba kwa miezi 18 sasa ndiye wa kulaumiwa wakishuka’