SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumamosi, 30 Aprili 2016

T media news

Lishe Bora kwa Maisha Yote

Inajulikana kabisa kuwa nyumba imara hujengwa kwa mchanganyiko wa vitu vingi. Nyumba hii huonekana nzuri na yenye kupendeza wakati wote na pia haimomonyoki kirahisi wakati wa mvua au upepo mkali. Nyumba imara hujengwa kwa mchanganyiko kama wa cementi, mchanga, kokoto, nondo n.k. mchanganyiko huu huwa katika kiwango sahihi, hii ni kwamba kuna kiasi au uwiano sahihi katika mchanganyiko huu. Kimojawapo kati ya hivi kikipelea au kuwa katika kiasi pungufu basi nyumba haitakuwa imara, vilevile kimojawapo kikizidi basi nyumba haitakuwa imara pia. Hivyo nyumba ili iwe imara ni lazima mchanganyiko huu uwe katika uwiano ulio sahihi.

Mpaka hapo swali linakujia, je mwili wako unajengwa na nini? je kuna uhitaji wa uwiano sahihi?
Mwili wa binadamu hujengwa kwa chakula. Chakula hicho ni lazima kiwe chakula bora au mlo kamili. Mlo kamili unajumuisha makundi matano ya vyakula ambayo ni: nafaka, mizizi na ndizi, kundi la pili: vyakula vyenye jamii ya kunde na vyenye asili ya wanyama, kundi la tatu: mbogamboga, kundi la nne:matunda, kundi la tano: mafuta na sukari.

Mwili unahitaji chakula chenye mchanganyiko wa makundi haya ya chakula ili kuwa na afya bora na iliyo imara kama inavyolinganishwa na nyumba imara. Inajulikana kuwa mchanga ukizidi katika tofali nyumba itamomonyoka nakuanguka au cementi ikipungua pia nyumba itamomonyoka na kuanguka. Hii ni sawa na ulaji kwa binadamu, chakula kikiwa hakina au kina kiwango kidogo cha baadhi ya makundi ya chakula yaliyotajwa hapo juu lazima mwili utakuwa dhoofu, hata makuzi yake hayatakuwa mazuri. Magonjwa yatokanayo na utapiamlo ndio chanzo kikuu cha mwili kuwa na afya mbaya. utapia mlo hutokana na lishe duni au lishe iliyozidi.

Lishe duni ni hali ya mwili kukosa baadhi ya virutubishi vinavyohitajika mwilini, kama vile protini, wanga, mafuta, vitamini na madini. Mwili ukikosa baadhi ya virutubishi hivi hushindwa kufanya kazi zake za kimebotali vizuri na kusababisha madhara mengine mengi. Vilevile mwili ukiwa na lishe iliyozidi husababisha madhara makubwa hii inatokana na kubadilika kwa baadhi ya kazi za seli na ogani mbalimbali mwilini.

Magonjwa ya utapia mlo ni kama vile: kwashakoo, marasmasi, marasmasi na kwashakoo, upungufu wa damu (Iron Deficiency Anaemia), tatizo la ukosefu wa vitamini C, tatizo la Ukosefu wa vitamini A, tatizo la ukosefu wa madini Joto, na magonjwa yatokanayo na lishe iliyozidi ni kama kisukari, presha, magonjwa ya moyo ambayo ndio tatizo kubwa linalowakumba hasa matajiri wanaojikita zaidi katika vyakula vyenye mafuta mengi na sukari.                                                  
                                           
  Kundi la chakula, chanzo chake, virutubishi vyake, na kazi yake mwilini  

   Nafaka, Mizizi na Ndizimchele, mahindi, mtama, ulezi, ngano, uwele, viazi vikuu, viazi vitamu, mihogo, magimbi, viazi mviringo, na NdiziVirutubishi: Wanga
Huupatia mwili nguvu za kuweza kufanya kazi

2.Vyakula vya aina ya mikunde na vyenye asili ya wanyamaMaharage, kunde, mbaazi, soya, karanga,njegere, njugu mawe,dengu, choroko, asili ya wanyama ni: nyama, mayai, samaki, dagaa, kumbikumbi, senene, maziwa na nzige.Virutubishi: Protini
Hujenga mwili. Huwezesha mwili kutengeneza seli nyingine.
3.Mboga-mboga
mchicha, majani ya kunde, majani ya maboga, kisamvu, matembele, spinachi, mgagani, mlenda, mnavu, mchunga, karoti, pilipili hoho, nyanya chungu, biringanya, bamia, kabichi, figiri, sukuma wiki na chainizi.Virutubishi: Vitamini na Madini
 Huupa mwili kinga imara dhidi ya maradhi mbalimbali.
4.Matunda
mapera, maembe, machungwa, papai, nanasi, zambarau, dhabibu, mapesheni, machenza, ubuyu, ukwaju, limaoVirutubishi: vitamini na madini
 Huupa mwili kinga dhidi ya maradhi.Husaidia kwa baadhi ya virutubishi kutumika kwa ufasaha zaidi mwilini.
5.Mafuta na Sukari
mafuta ya kupikia, ufuta, karanga, mbegu za alizeti, siagi, samli, nyama yenye mafuta, sukari ni: asali, miwa, vyakula vinavyotengenezwa kwa sukari nyingi kama jamu, keki, n.kvirutubishi: mafuta
Huupa mwili nguvu.Husaidia ufyonzwaji wa vitamini A,D,E na K.

Maji???????

Maji hayakuwekwa kwenye kundi lolote la chakula kwa sababu hayana virutubishi. Ni muhimu kunywa maji safi na salama kwani yanarahisisha umeng'enyaji wa chakula, kusafirisha virutubishi na kutoa uchafu ambao hutengenezwa mwilini wakati mwili unafanya kazi zake. Asilimia kubwa ya mwili ni maji hivyo ni vyema kunywa maji mara kwa mara ili kuwa na afya bora.

Kumbuka:

ni vema kula vyakula vyenye mchanganyiko wa kila kundi la chakula ili mwili uwe na afya nzuri, na kutopatwa na maradhi mara kwa mara, pia kunywa maji safi na salama wakati wote unapohitaji.

 

              







Magonjwa na Matatizo ya Utapiamlo

Utapia mlo ni hali ya kuwa na lishe duni au iliyozidi ambayo huambatana na matatizo mbalimbali ya kiafya. ni hali inayotokana na kula chakula chenye virutubishi visivyotosheleza au virutubishi vilivyozidi kana kwamba kinasababisha matatizo ya kiafya. ulaji wa vyakula vyenye virutubishi kidogo au pungufu hutokana na ulaji usiohusisha makundi matano ya vyakula, kwa mfano watanzania wengi hula vyakula vya aina moja kwa mida tofauti, mfano zaidi: asubuhi labda amekunywa uji, mchana akala ugali,makande au wali, jioni akala ugali au pilau. hii inaonyesha kuwa mlaji amekula chakula kilekile kwa kubadili mapishi tu, yaani badala ya uji akala ugali au makande, badala ya wali akala pilau, hapa atakuwa amekula virutubishi vya aina moja mara kwa mara. ulaji huu husababisha mwili kukosa baadhi ya virutubishi na kupelekea magonjwa na matatizo ya utapiamlo.
Vilevile ulaji unaozidi kiwango husababisha virutubishi kuzidi mwilini na kujikusanya katika sehemu mbalimbali za mwili. kujikusanya kwa virutubishi hivi huweza kubadili kazi za seli au mifumo mbalimbali ya mwili. ulaji wa vyakula vya mafuta mengi na sukari au vyakula vinavyopikwa kwa mafuta mengi ndio chanzo kikubwa cha mtu kuwa na mkusanyiko wa mafuta mwilini na kuwa na uzito uliozidi. vyakula kama chipsi, nyama choma, soda, vyakula vinavyopikwa kwa mda mfupi (fast foods), sukari, biskuiti, jam, keki, n.k.

Yafuatayo ni magonjwa na matatizo ya utapiamlo:
A: Kwashakoo
kwashakoo ni ugonjwa utokanao na ukosefu wa viini vya protini mwilini. mara nyingi ugonjwa huu huwapata watoto. ugonjwa huu hutokana na kula vyakula visivyokuwa na kundi la chakula yaani chakula chenye jamii ya kunde na vyenye asili ya wanyama.

Dalili:
-ngozi na nywele hubadilika rangi na kuwa na wekundu-wekundu (reddish-orange)
-mwili kujaa maji (huonekana mnene/amevimba)
-ngozi hupauka na kuwa inatoa ukurutu.
-huharisha
-mchovu
-hana hamu ya kula
-anazubaa zubaa

B:Marasmasi.
Marasmasi ni ugonjwa utokanao na ukosefu wa viini vya wanga mwilini. hii huchangiwa na kutokula chakula chenye viini vya wanga hasa kundi la chakula la Nafaka, Mizizi, na Ndizi, mara nyingi ugonjwa huu huwapata watoto.

Dalili:
-unyafuzi uliozidi
-ngozi hukauka
-baadhi ya sehemu za mwili husinyaa na kuning'inia (matako, korodani, kwapa)
-ngozi huvutika sana (tishu za ngozi huwa hazina mafuta)
-huonekana amekonda sana.
-anahamu kubwa ya kula.
-uso huwa kama wa nyani/mdogo 
-macho yao huwa makubwa
-tumbo lao huwa limevimba
-hulia mara kwa mara
-ngozi imekauka/sinyaa
-nyuso zao ni nyembamba/ndogo.

C: Marasmasi na kwashakoo.
Ugonjwa huu hutokana na ukosefu wa viini vya protini na wanga mwilini kwa pamoja. Yaani kutokula chakula chenye makundi ya chakula ambayo kundi la kwanza ni vyakula vyenye jamii ya kunde na vyenye asili ya wanyama, na la pili ni vyakula vya Nafaka, Mizizi na Ndizi. Pia ugonjwa huu mara nyingi huwapata watoto. 

Dalili:
-Ugonjwa huu huonyesha dalili zote za ugonjwa wa marasmasi na kwashakoo kwa pamoja kama zilivyoainishwa awali.
-mtoto mwenye magonjwa haya kwa pamoja yuko katika hatari ya kifo.

D: Tatizo la Ukosefu wa vitamini A. (ukavu macho)
tatizo hili husababishwa na kutokula chakula chenye vitamini A kama vile mbogamboga na matunda, inajulikana kuwa matunda na mbogamboga zenye rangi ya njano/machungwa vina vitamini A kwa wingi zaidi. viazi vya njano (viazi lishe), na karoti zina vitamini A nyingi zaidi. mbogamboga zingine pamoja na matunda pia yana vitamini A nyingi. Vitamini A hufonzwa kwa ufasaha zaidi chakula kikiwa na mafuta kiasi.
Dalili:
-macho kukauka
-macho kuwa na ukungu/weupe (hali ikiwa imekithiri)
-kutoona vizuri hasa wakati wa usiku

E: Tatizo la Ukosefu wa Madini Chuma (Iron Deficiency Anaemia)
Tatizo hili huwapata sana watoto na wanawake, pia watu katika makundi mengine hupatwa na tatizo hili. Tatizo hili husababishwa na kutokula chakula chenye viini vya madini ya chuma kama vile mbogamboga, nyama, mayai, juisi ya rosella, n.k, pia utumiaji wa vidonge vya madini ya chuma kama inavyoshauriwa na dakitari huongeza damu. malaria na minyoo husababisha upungufu wa damu pia. madini chuma hufonzwa kwa ufasaha panapokuwepo na chakula chenye vitamini C kama ubuyu, ukwaju, machungwa, limao, n.k. hivyo ni vema kula vyakula vyenye madini chuma pamoja na vyenye vitamini C ili kuwezesha ufyonzwaji wa madini chuma kwa ufasaha zaidi. Epuka vizuizi vya madini chuma katika ufyonzwaji wake kama vile kahawa, chai, ugoro, tumbaku, na vinywaji vya cocacola kwa saa moja kabla au baada ya kula chakula chenye madini chuma. zuia ugonjwa wa malaria kwa kulala kwenye chandarua, kutibu malaria haraka baada ya kuugua, pata vidonge vya kujikinga na malaria (SP) hasa wajawazito. jikinge na minyoo kwa kuvaa viatu, meza vidonge vya minyoo mara mbili kwa mwaka, tumia vyoo kujisaidia haja kubwa na ndogo na osha mikono kabla na baada ya kula.

Dalili:
-Sehemu za mwili huwa nyeupe zaidi, kama vile ulimi, kucha, ngozi hupauka, lips, sehemu za macho, na fizi
-kizunguzungu
-kuchoka
-kuumwa na kichwa

F: Tatizo la Ukosefu wa Madini Joto (Iodine Deficiency Disorder)
Tatizo hili husababishwa na kutokula chakula chenye madini Joto. madini joto hupatikana kwenye chumvi yenye madini joto (iodized salt), hasa chumvi hii hupatikana madukani. Ugonjwa ujulikanao kama Goita ndio husababishwa na ukosefu wa madini Joto.

Dalili
-Tezi za/shingo kuvimba