Rais Hassan Rouhani ameutaka Umoja wa Ulaya utoe ushirikiano katika mapambano dhidi ya ugaidi na kusisitizia ulazima wa kutekelezwa ipasavyo makubaliano ya nyuklia (JCPOA).
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa wito huo leo katika mazungumzo na Rais wa Baraza la Seneti la Ubelgiji Bi Christine Defraigne ambaye yuko safarini hapa nchini.
Rais Rouhani ameashiria mchango chanya wa Umoja wa Ulaya katika makubaliano ya nyuklia baina ya Iran na nchi zinazounda kundi la 5+1 na kueleza kwamba: makubaliano ya nyuklia ni mwanzo tu wa safari na si mwisho wake; na kitu pekee cha kuifanya mihimili ya makubaliano hayo iwe imara zaidi ni kutekelezwa kwa wakati na kama inavyopasa makubaliano na ahadi zilizotolewa.
Rais Rouhani amebainisha kuwa ugaidi ni tatizo kubwa na sugu linaloukabili ulimwengu; na mbali na kubainisha sababu na chanzo chake amesisitiza kuwa pamoja na sababu za kiuchumi na kiutamaduni kama umasikini, ujinga, ubaguzi na kukata tamaa vijana juu ya mustakabali, lakini malalamiko na upinzani wa vijana hao dhidi ya uingiliaji wa madola ya kigeni katika nchi zao nayo pia ni miongoni mwa vyanzo na sababu kuu za kujitokeza ugaidi. Amesisitiza kuwa mashambulio ya kijeshi na udondoshaji makombora si utatuzi wa msingi wa kupambana na ugaidi, bali inapasa kutumia suhula zote ili kutokomeza chimbuko na sababu za kujitokeza ugaidi.
Kwa upande wake, Rais wa Baraza la Seneti la Ubelgiji ametaka kufunguliwa ukurasa mpya katika uhusiano wa nchi yake na Iran na kueleza kwamba Brussels iko tayari kushirikiana na Tehran katika nyanja zote.
Kabla ya kukutana na kufanya mazungumzo na Rais Rouhani, Rais wa Baraza la Seneti la Ubelgiji alikutana na kufanya mazungumzo pia na Waziri wa Mambo ya Nje, Muhammad Javad Zarif.