SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumamosi, 30 Aprili 2016

T media news

Tume ya uchaguzi DRC yataka muda zaidi kujitayarisha kwa ajili ya uchaguzi

Tume Huru ya Uchaguzi Katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (CENI) imeomba muda zaidi wa kujitayarisha kwa ajili ya kuandaa zoezi la uchaguzi wa rais.

Mkuu wa CENI Corneille Nangaa amesema anahitaji takribani miezi 16 ili kuandaa kwa njia sahihi uchaguzi ujao wa rais nchini humo. Akizungumza mjini Kinshasa, Nangaa amesema tume hiyo inapaswa kuandikisha wapiga kura na kutayarisha daftari jipya la wapiga kura na kwamba zoezi hilo linahitaji miezi 16.

Aidha mkuu wa Tume Huru ya Uchaguzi DRC amesema tume hiyo imewasilisha ombi hilo kwa Umoja wa Mataifa na kwamba azimio 2277 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilihusu ombi hilo. Azimio hilo lilitaka serikali ya DRC iandae uchaguzi wa rais kwa mujibu wa katiba ya nchi.

Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo anakamilisha duru yake ya urais tarehe 19 Desemba mwaka 2016. Pamoja na hayo tume ya uchaguzi nchini humo inasema inahitajia zaidi ya dola bilioni moja ili kuandaa uchaguzi wa rais kwa mafanikio.

Tangazo hilo la CENI linakuja huku kukiwa na malumbano ya kisiasa DRC kuhusu uamuzi wa Kabila kugombea urais.

Weledi wa masuala ya sheria wanasema kuwa, kwa mujibu wa katiba ya DRC, Kabila hana haki ya kuwa mgombea katika duru ijayo ya uchaguzi wa rais. Hii ni katika hali ambayo Kabila anajitayarisha kutetea kiti chake katika uchaguzi huo.

Joseph Kabila aliingia madarakani siku 10 baada ya kuuawa baba yake, Laurent-Désiré Kabila mwezi Januari 16 mwaka 2001. Alitawala bila kuchaguliwa kwa kura za wananchi. Kufuatia mashinikizo ya kitaifa na kimataifa, uchaguzi wa kwanza huru wa rais nchini humo ulifanyika mwaka 2006 ambapo Kabila alisinda katika uchaguzi huo. Katika uchaguzi wa pili wa mwaka 2011, Kabila alipata ushindi na hivi sasa pia akipata njia, anaweza kubakia madarakani hadi mwaka 2021.

Ingawa wenzake katika nchi zingine za Afrika wamebadilisha katiba na kubakia madarakani, inaelekea kuwa Kabila atatumia mbinu nyingine kubakia madarakani.

Kufuatia kuongezeka mgogoro wa kisiasa nchini DRC, Kabila ametoa pendekezo la kufanya mazungumzo na wapinzani lakini ombi lake hilo limekataliwa na wapinzani ambao wamelitaja kuwa ni njama yake ya kutaka kusalia madarakani.

Wapinzani wa Joseph Kabila wanasema anatafuta njia za kuongeza muda wake madarakani kwa miezi kadhaa ili kwa njia hiyo atafute mbinu za kumuwezesha kuendelea kuitawala nchi hiyo milele.

Vyama vya upinzani vinasisitiza kuwa uchaguzi DRC lazima ufanyike katika kipindi kilichoainishwa. Wapinzani wanasema iwapo pendekezo la tume ya uchaguzi la kuandikisha upya wapiga kura litakubaliwa, basi zoezi hilo litachukua zaidi ya miezi 16 iliyotajwa na tume hiyo.

Katika upande mwingine kuendelea machafuko mashariki mwa DRC kunatajwa kuwa sababu nyingine ambayo inaweza kutumiwa na serikali ya Kinshasa ili Kabila aendelee kubakia madarakani. Wapinzani wanalalamikia utendaji kazi wa Kabila na wanasema kuendelea kubakia kwake madarakani kutapelekea nchi hiyo kutawaliwa kidikteta.

Wapinzani hivi sasa wanasisitiza kuwa lazima Kabila aondoke madarakani sambamba na kufanyika mabadiliko katika muundo wa kisiasa DRC. Aidha wanasisitiza kuhusu uchaguzi huru kufanyika katika kipindi kilichoainishwa kisheria.