SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumamosi, 30 Aprili 2016

T media news

Wapinzani Chad wataka kubatilishwa matokeo ya uchaguzi wa Rais

Wapinzani nchini Chad wamelitaka Baraza la Katiba la nchi hiyo kubatilishwa matokeo ya uchaguzi wa Rais yaliyomrejesha tena madarakani Rais Idriss Deby.

Wapinzani sita waliowania kiti cha Urais katika uchaguzi wa hivi karibuni nchini Chad wametangaza kuwa, wamelitaka Baraza la Katiba litengue matokeo ya uchaguzi huo kwani zoezi zima la uchaguzi huo lilitawaliwa na wizi wa kura na udanganyifu.

Joseph Djimrangar Dadnadji, Waziri Mkuu wa zamani wa Chad ametangaza kuwa, suala la kukiukwa sheria katika kipindi cha kufanyika uchaguzi na wakati wa zoezi la kuhesabu kura linatosha kubatilisha matokeo ya uchaguzi.

Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa na Tume Huru ya Uchaguzi ya Chad, Rais Deby alipata asilimia 61.56 ya kura katika uchaguzi uliofanyika tarehe 10 ya mwezi huu na hivyo kupata fursa ya kuiongoza tena nchi hiyo kwa kipindi kingine cha miaka mitano.

Wakati wapinzani wakitoa malalamiko hayo, wiki iliyopita waangalizi wa Umoja wa Afrika kwenye uchaguzi huo walinukuliwa wakisema kuwa, uchaguzi wa Rais nchini Chad ulifanyika katika anga huru na salama. Rais Déby amekuwa madarakani tangu mwaka 1990, baada ya kumuondoa madarakani aliyekuwa rais wa nchi hiyo, dikteta Hissène Habré.