SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumamosi, 30 Aprili 2016

T media news

Kiongozi wa upinzani nchini Bahrain aachiliwa huru baada ya kutumikia kifungo cha miaka mitano jela

Sheikh Mohammed Ali Mahfoudh, Katibu Mkuu wa Chama cha Amalul-Islami nchini Bahrain ameachiliwa huru baada ya kutumikia kifungo cha miaka mitano jela.

Mahakama moja ya utawala wa kifalme wa ukoo wa Aal -Khalifa ilikuwa imemhukumu Sheikh Mahfoudh kifungo cha miaka kumi jela, lakini mnamo mwezi Novemba mwaka 2012 mahakama ya rufaa ilitoa uamuzi wa kupunguza adhabu ya kifungo hicho kutoka miaka kumi hadi mitano.

Katibu Mkuu huyo wa Chama cha Amalul-Islami alifungwa jela kutokana na malalamiko yaliyotolewa na Waziri wa Sheria wa Bahrain dhidi ya chama hicho.

Tangu mwezi Februari mwaka 2011, wananchi wa Bahrain wamekuwa wakifanya maandamano ya amani nchini kote kupinga utawala wa kidikteta wa kifalme wa ukoo wa Aal Khalifa na kuutaka ung'atuke madarakani.

Utawala huo umekuwa ukitumia mkono wa chuma kukabiliana na maandamano hayo sambamba na kutekeleza sera za kibaguzi dhidi ya Waislamu wa madhehebu ya Shia ambao ndio wanaounda asilimia kubwa ya wananchi wa Bahrain.

Mamia ya watu wameuawa, kujeruhiwa au kutiwa nguvuni na askari wa utawala wa Aal Khalifa.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yamekuwa yakiulaumu vikali utawala huo kutokana na adhabu za vifungo vya muda mrefu jela unaotoa dhidi ya wapinzani mbali na kuwavua uraia baadhi ya wapinzani hao.