Mapigano yameanza tena kati ya jeshi la Sudan na waasi katika eneo la Kordofan Kusini.
Arnu Lodi, msemaji wa waasi wa eneo la Kordofan Kusini ametangaza leo kuwa wapiganaji saba wa kundi hilo la waasi wameuawa na wengine kadhaa wamejeruhiwa katika mapigano hayo. Mwezi mmoja umepita tangu yalipotokea mapigano kwa mara ya mwisho baina ya jeshi la serikali ya Khartoum na waasi wa eneo la Kordofan Kusini.
Kwa mujibu wa jeshi, mapigano baina ya pande hizo mbili yalianza siku ya Jumatano katika mji wa Oum Sediba.
Tangu mwaka 2011 hadi sasa waasi katika majimbo ya Kordofan Kusini na Blue Nile wanapambana na jeshi la serikali ya Khartoum katika majimbo hayo.
Mwishoni mwa mwaka jana Rais Omar al-Bashir alitangaza dikrii ya kusitishwa vita katika maeneo hayo na akarefusha muda wa dikrii hiyo kwa muda wa mwezi mmoja.
Watu zaidi ya milioni mbili wamebaki bila ya makaazi katika eneo la kusini mwa Sudan kutokana na mapigano na machafuko yaliyolikumba eneo hilo..