Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Masiliano Ofisi ya Bunge, Owen Mwandumbya akizungumza na wanahabi mjini Dodoma jana akitoa taarifa ya yale yatakayojiri katika Mkutano wa sita wa Bunge la 11 unaotaraji kuanza leo Januari 31 hadi Februari 10 mwaka huu mjini Dodoma.
Mkutano wa Sita wa Bunge unatarajiwa kuanza siku ya Jumanne tarehe 31 Januari 2017 na kumalizika tarehe 10 Februari 2017 Mjini Dodoma.
Mkutano huo utakuwa ni mahususi kwa ajili ya kupokea Taarifa za mwaka za Kamati za Kudumu za Bunge ambapo Kamati 14 za kisekta na mtambuka zitawasilisha taarifa zake Bungeni katika kipindi hiki. Shughuli nyingine zitakazofanyika katika Mkutano huu ni kama ifuatavyo:-
1.0 KIAPO CHA UAMINIFU
Kufuatia uteuzi wa wabunge watatu walioteuliwa na Mhe. Rais Dk. John Pombe Magufuli hivi karibuni na Uchaguzi Mdogo uliofanyika katika Jimbo la Dimani, Zanzibar Tarehe 22 Januari 2017, kutakuwa na Kiapo cha Uaminifu kwa Wabunge wapya wanne ambao ni:-
(i) Mhe. Alhaji Abdallah Majula Bulembo
(ii) Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi
(iii) Mhe. Anne Kilango Malecela
(iv) Mhe. Ali Juma Ali - (Jimbo la Dimani)
2.0 MASWALI
Katika Mkutano huu jumla ya maswali ya kawaida 125 yanatarajiwa kuulizwa na kujibiwa Bungeni. Aidha, kwa mujibu wa Kanuni ya 38 (1) ya Kanuni za Kudumu za Bunge wastani wa maswali 16 ya papo kwa papo kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu yataulizwa na kujibiwa pia siku za Alhamisi.
3.0 KAULI ZA MAWAZIRI
Aidha, katika Mkutano huu wa Bunge Kauli mbili za Mawaziri zitawasilishwa kama ifuatavyo:-
(i) Kauli ya Serikali Kuhusu Hali ya Chakula Nchini itakayotolewa Tarehe 31 Januari, 2017.
(ii) Kauli ya Serikali kuhusu Deni la Taifa na Hali ya Uchumi Nchini itakayotolewa Tarehe 31 Januari, 2017.
4.0 MISWADA YA SHERIA
Katika Mkutano wa Tano wa Bunge uliomalizika mwezi Novemba, 2016 Miswada mitatu (3) ya Sheria ilisomwa kwa mara ya Kwanza Bungeni na kupelekwa kwenye Kamati husika ili ifanyiwe kazi.
Hivyo katika Mkutano huu wa Sita Miswada hiyo inatarajiwa kuwasilishwa Bungeni kwa mara ya Pili, kujadiliwa na kupitishwa na Bunge kwa mujibu wa Kanuni ya 91. Miswada hiyo ni:-
Muswada wa Sheria ya Sheria ya Madaktari wa Meno na Wataalam wa Afya Shirikishi wa mwaka, 2016 (The Medical, Dential and Allied Health Professionals Bill 2016).
Muswada wa Sheria ya Huduma ya Msaada wa Kisheria wa mwaka 2016 (The Legal Aid Bill, 2016).
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali (Na.4) wa mwaka 2016. {The Written Laws (Miscellaneous Amendments)}, Bill, 2016)
Imetolewa na:
Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano
Ofisi ya Bunge
DODOMA
30 Januari, 2017.