Ama kweli imeshangaza wengi! Kitendo cha nyota wa muziki wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond’ na Ally Saleh Kiba kushindwa kutokeza kwenye sherehe za kumbukumbu ya kuzaliwa Mtume Muhammad (S.A.W), yaani Maulidi iliyofanyika wilayani Temeke jijini hapa ambapo walialikwa na Shehe Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum na kumuahidi kuwa wangefika.
Katika Maulidi hiyo ambayo ilifanyika Mtaa wa Liganga wilayani hapo na mwenyeji wa shughuli hiyo kuwa Shehe Alhad, ilihudhuriwa na waheshimiwa mbalimbali wakiwemo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Idd, Makamu wa Rais Mstaafu wa Tanzania, Dk. Mohammed Gharib Bilal, Mufti wa Tanzania, Shehe Abubakar Zubeir na wengineo.
KAULI YA SHEHE MKUU JUKWANI
Wakati Maulidi hiyo ikiendelea, Shehe Alhad aliutangazia umati uliojaa kuwa, katika hafla hiyo aliwaalika wasanii mbalimbali na kuwataka watu kuwachukulia wasanii hao kama wenzao. Akiendelea kuweka mambo sawa, alisema mpaka muda huo msanii ambaye alishafika ni Ahmed Olotu ‘Mzee Chilo’ na pia akaongeza kuwa, msanii wa nyimbo za kughani, Mrisho Mpoto ‘Mjomba’ alikuwa njiani kufika eneo la tukio ingawa mpaka wageni waalikwa wanaondoka, Mpoto alikuwa hajafika.
Baadhi ya watu walifurika kwenye eneo hilo na kujua kuwa, Diamond na Kiba wangekuwepo, walishangaa kuona muda unakwenda bila wapendwa hao kuonekana licha ya kusubiriwa kwa hamu kubwa.
KAMA WANGEFIKA
Baadhi yao walisema kuwa, kama Diamond na Kiba wangejitokeza kwenye Maulidi hiyo, wanaamini Shehe Alhad angewaunganisha na kuwashikanisha mikono ya wengine wakiwa hawezi hata kuongea.
WAGENI WAALIKWA WAONDOKA
Baada ya Shehe Alhad kuwasindikiza wageni waalikwa, Wikienda lilimuweka chemba na kuanza kumuhoji kuhusiana na kutofika kwa Diamond na Kiba ambao ilisemekana aliwaalika. “Aaah! Ni kweli Diamond na Kiba niliwaalika na wote waliniahidi kufika lakini nashangaa mpaka muda huu hawajatokea, sijui ni kwa nini lakini hilo siwezi kulizungumzia zaidi isipokuwa hata mimi nashangaa,” alisema Alhad na kuomba aachwe aendelee na majukumu yaliyombana, ikiwemo
kuagana na wageni wengine. Wikienda liliwapigia simu Diamond na Kiba ili kutaka kujua kilichowasibu mpaka kushindwa kutokea kwenye mwaliko huo.
DIAMOND: “Ni kweli nilialikwa, lakini nilipata dharura ya kifamilia, niko Afrika Kusini.”
Kiba simu yake haikuwa hewani.