Mara nyingi vitendo vya ukatili na unyanyasaji kijinsia vimezoeleka kufanywa na wanaume dhidi ya wanawake na watoto.
Hata hivyo, kampeni ya “Tunaweza” inayoratibiwa na shirika lisilo la kiserikali la Kivulini jijini Mwanza kwa lengo la kutokomeza ukatili na unyanyasaji wa kijinsia, imebaini kuwa vitendo hivyo pia hufanyika dhidi ya wanaume.
Mkazi wa Mtaa wa Mwananchi, Kata ya Mahina jijini Mwanza, Ernest Kibinzaroya (78) ni mfano wa ukatili unaofanywa na wanawake dhidi ya wanaume. Yeye pamoja na mkewe, Maria Kibinzaroya (57) wamejitokeza hadharani kueleza walivyopitia maisha hayo.
Inaelezwa kwamba Maria alikuwa akimpa kipigo cha mara kwa mara mumewe kabla ya ‘kuokoka’ na kuwa mke mwema.
‘Wokovu’ huo ni baada ya kampeni hiyo inayofanyika katika wilaya za Ilemela, Nyamagana, Magu, Misungwi, Sengerema mkoani Mwanza kuwafikia wanadoa hao na wote hivi sasa wana mabadiliko na wanapiga vita ukatili na unyanyasaji wa kijinsia.
Akizungumza mbele ya mumewe wakati wa mahojiano maalumu nyumbani kwao, Maria anasema miaka zaidi ya 30 ya ndoa yao imekuwa ya mateso, manyanyaso na misukosuko iliyoambatana na kipigo alichokuwa akimpa mumewe.
“Kabla ya kupata elimu kuhusu vita dhidi ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia, nilikuwa nampiga mume wangu mara kwa mara,” anasimulia Maria.
Huku mume wake akitikisa kichwa kuonyesha kukubaliana na maelezo ya mkewe, Maria anasema vitendo hivyo viliambatana wakati mwingine na kugoma kupika chakula, vimemfanya mumewe kupata shinikizo la damu.