SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumamosi, 28 Januari 2017

T media news

Ni Funzo Kubwa…. Liruhusu Likae Moyoni Mwako

nomaKuna jamaa alikuwa masikini sana mkoani Kigoma. Alikuwa akiishi na mke wake huku wakiwa na mtoto wao mdogo. Kutokana na maisha kuwa magumu, akaamua kuwa mkulima. Akalima na kulima lakini hakufanikiwa. Akakata tamaa hivyo kuamua kujiingiza kwenye uuzaji wa mafuta ya mawese.

Alihisi kwamba mambo yangebadilika lakini baada ya yeye kuanza biashara hiyo, soko la mafuta ya mawese likashuka kwa kasi ya ajabu hivyo hakufanikiwa. Maisha yaliendelea kumtesa, umasikini ulimtafuna yeye na familia yake.

Kikafika kipindi akachoka, hakutaka kuona akiteseka na familia yake hivyo kumwambia kwamba ni lazima aondoke na kwenda nchini Kongo kuchimba dhahabu, labda bahati yake ilikuwa huko. Mkewe alipinga lakini akamshawishi kwa kipindi kirefu na hatimaye akakubaliana naye.

Baada ya kutafuta fedha za kuungaunga, akaelekea huko. Alipofika, alikaa kwa miaka saba ndipo akafanikiwa kupata dhahabu kubwa, nzito ambayo aliamua kuibeba katika begi lake na kurudi Kigoma kwa meli.

Ndani ya meli kulikuwa na watu wengi, hasa Wazungu ambao walikwenda huko kufanya utalii. Wakati meli ikiwa imefika katikati ya ziwa Tanganyika, ikaanza kuzama. Watu walipiga kelele sana, kwa jamaa hakukuwa na tatizo kwani alijua sana kuogelea, hivyo akawa anapiga mbizi na wakati mwingine kuelea juu ya maji.

Wakati watu wengi wamekufa, akasikia sauti ya msichana mmoja mdogo akilia, alikuwa mtoto wa Kizungu, wa kike aliyekuwa akiomba msaada. Jamaa alimuona mtoto yule wa miaka kumi na tano, akaamua kumfuata na kumbeba, kitu cha ajabu kabisa ambacho hakujua ilikuwaje, akaanza kuzama kutokana na uzito.

Kulikuwa na mambo mawili makubwa, alitakiwa kufanya moja ili anusurike. La kwanza lilikuwa ni kumuacha mtoto yule afe na yeye aondoke zake, au kuiacha dhahabu ile ili amnusuru yule mtoto. Ulikuwa mtihani mkubwa mno kwake. Aliondoka nyumbani miaka saba iliyopita, alimwambia mkewe kwamba anakwenda kutafuta utajiri nchini Kongo.

Alifanikiwa kwa kupata dhahabu kubwa ambayo aliamini ingemfanya kuwa bilionea. Sasa iweje aiache dhahabu kwa ajili ya mtoto asiyemjua ambaye wazazi wake walikufa? Moyo wake ukagawanyika, upande mmoja ukamwambia aachane na mtoto kwani hata angemuokoa, angeishi naye wapi?

Angemsaidia nini na wakati hawakujuana? Ukamkumbusha maisha aliyokuwa amepitia, maisha ya kimasikini, yaliyomuumiza, yakamletea picha ya mkewe na mtoto wake walivyokuwa wakiteseka kwa kupigwa na umasikini.

Upande mwingine ukamwambia lilikuwa jambo jema kumsaidia mtoto yule. Utajiri hauna kitu mbele ya utu. Ilikuwa ni lazima amsaidie mtoto yule kwani hata kama angepata fedha, bado angekufa baadaye, ni wangapi walikuwa na fedha ila wamekufa na kuziacha fedha hizo?

Moyo wake ukawa mgumu kufanya maamuzi lakini mwisho wa siku akaitupa dhahabu kubwa majini. Moyo ulimuuma sana lakini hakuwa na jinsi. Akambeba msichana yule wa Kizungu na kuanza kuogelea naye, saa moja mbele, wakaokolewa na meli nyingine.

Mtoto yule akasaidiwa na Umoja wa Mataifa kurudishwa Marekani alipokuwa akiishi huku nyuma jamaa alipofika nyumbani na kumuhadithia mkewe kilichotokea, alimtukana sana na kumuona mjinga, iweje atupe dhahabu na wakati alipoteza miaka saba kuitafuta? Majirani wakamcheka, wakamdharau na mkewe akaamua kuondoka kurudi kwao kwani asingeweza kukaa na mwanaume mpumbavu kama yeye.

Jamaa akaanza upya, maisha yakaanza kumpiga tena. Alilia sana, alichekwa kila kona. Alitamani kurudi Kongo kutafuta tena dhahabu lakini hakuwa na fedha. Akawa ombaomba, kila kona mkoani Kigoma alikuwa akipita kuomba, kuanzia Ujiji, Mwanga, Mwembetogwa, Mji Mwema, Bangwe na kila sehemu alikuwa akiombaomba.

Baada ya miaka mitano, wakati akiwa amepigwa sana na maisha, ghafla akamuona msichana wa Kizungu akija mbele yake. Hakumjua, msichana yule alipiga hatua mpaka kule nyumbani kwake alipokuwa. Alipofika, akamsalimia huku akiwa na Mkalimani wake. Akamuuliza kama alimkumbuka, jamaa akasema hamkumbuki ndipo yule msichana akasema kwamba yeye ndiye yule binti wa miaka kumi na tano aliyekuwa amemuokoa kipindi cha nyuma.

Jamaa alifurahi kumuona, akamkumbatia. Msichana yule akamwambia kwamba alikuwa akimkumbuka kila siku kwa wema aliomuonyeshea. Kipindi hicho, msichana huyo alifanikiwa sana, alikuwa mfanyabiashara mkubwa Marekani, mwenye kampuni nyingi kwani wazazi wake walimuachia utajiri mkubwa.

Jamaa akamwambia kila kitu kilichotokea katika miaka mitano ya mateso. Msichana yule akahuzunika sana, alichokifanya ni kumwambia jamaa kwamba alikuja Kigoma kwa ajili ya kumchukua yeye na familia yake kwenda kuishi nchini Marekani kama fadhila kwake. Ila kwa sababu mkewe aliondoka na mtoto na hakujua walipokuwa, basi aondoke naye tu.

Jamaa akafurahi. Huo ndiyo ukawa mwisho wa kuishi Tanzania. Akaondoka na kuelekea Marekani, kama alivyokuwa msichana yule, naye akawa mfanyabiashara mkubwa. Ameoa huko na maisha yake yanaendelea kama kawaida.

FUNZO: Unapotakiwa kutenda wema, wewe tena pasipo kujali itakugharimu kiasi gani. Inawezekana jamaa angeona dhahabu ni mali, angekufa njiani au ingepotea. Kwa kumsaidia msichana yule, Mungu akaileta meli. Kwa kumuokoa msichana yule, leo hii yupo nchini Marekani akila maisha.

Alisubiri kwa miaka mitano, kama kukata tamaa angekata mapema sana. Msichana hakumsahau, aliendelea kumkumbuka, aliukumbuka wema wake na kurudi Tanzania kutoa fadhila.

E.J SHIGONGO.