SERIKALI imetangaza kuwasaka na kuwafikisha katika vyombo vya dola wafanyabiashara wa mitaani wanaokopesha fedha kwa riba bila kuwa na leseni ya biashara hiyo.
Pamoja na wafanyabiashara hao, Waziri wa Katiba na Sheria Dk Harrison Mwakyembe ameomba wananchi wasaidie kuwafichua polisi na Mahakimu wanaowapa nguvu wafanyabiashara hao kinyume na sheria.
Akizungumza na wanahabari jana mjini Iringa, Dk Mwakyembe alisema baada ya kuwasili mjini Iringa juzi kikazi aliwafuata akinamama watano waliolalamikia watu binafsi wenye fedha wanaofanya biashara hiyo ambao walilalamika kutozwa riba kwa mikopo wanayochukua jambo linalowatia umasikini.
Dk Mwakyembe alisema kwa mujibu wa sheria namba 5 ya 2006 ni kosa la jinai kwa mtu yoyote kufanya biashara ya kukopesha fedha bila kuwa na leseni ya biashara hiyo inayotakiwa kulipiwa kodi.
“Baada ya kufikishwa mahakamani na kupatikana na hatia, adhabu kwa mtu anayepatikana na kosa hilo ni ama kifungo cha miaka mitano jela au faini ya shilingi milioni 20,”alisema.
Wakati sheria hiyo ikiwa wazi, alisema amepokea taarifa kutoka kwa akinamama hao kwamba wapo baadhi ya polisi wa mjini Iringa kwa sababu wasizozifahamu wamekuwa wakizifanya kesi zinazohusu mikopo hiyo kuwa za jinai badala ya madai.
“Pamoja na askari hao kuna Mahakimu, wanaoshirikiana na wafanyabiashara hao kutengeneza mikataba ya mikopo hiyo na kusimamia kesi zake pale, waombaji wa mikopo wanaposhindwa kulipa,” alisema.
Alisema kwa nguvu ya askari na Mahakimu hao, wanaoshindwa kulipa mikopo hiyo hunyang’anywa mali zao na watu wenye benki hizo alizoziita benki kanjanja na kuuzwa kwa watu wengine jambo linalozidisha umasikini kwa wajasiriamali hasa wanawake.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza alisema taarifa hizo hazijawahi kufikishwa ofisini kwake na ataitumia taarifa hiyo ya waziri kutoa maelekezo ya kuzishughulikia.