SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumanne, 31 Januari 2017

T media news

CCM - Chadema Wanasababisha Migogoro ya Ardhi..!!!


MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa Wilaya ya Monduli mkoani Arusha, Loota Sanare amesema halmashauri ya wilaya hiyo inayoongozwa na Chadema, inachochea migogoro ya ardhi na chama hakitakaa kimya kwa hilo.

Sanare alisema hayo juzi katika mkutano wa hadhara wa kijiji cha Lendikinya, uliohudhuriwa na vijana wa jamii ya Kimasai (morani) na wazee wa mila (Laigwanani) zaidi ya 300, kueleza ardhi ya kijiji hicho inayotaka kunyang’anywa na halmashauri hiyo.

Alisema vijana wa kimorani, Laigwanani na watu wengine akiwemo yeye mwenyewe Sanare, wanamiliki ardhi iliyopo katika kijiji hicho kwa kufuata michakato yote ya kisheria na hatimaye kupata hati ya kumiliki ardhi.

Alisema amesikitishwa na kauli ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli, Isack Joseph kutangaza baadhi ya watu kuwa wanamiliki ardhi katika msitu huo kinyume cha sheria.

Alisema CCM haitavumilia uchochezi unaofanywa na baadhi ya viongozi wa halmashauri kwa maslahi binafsi.

Pia, alisema CCM haitavumilia kuona mwananchi yeyote anaonewa.

Sanare alisema yeye alipata shamba hilo kama mwananchi wa kijiji hicho na hakuchukua shamba hilo kama kiongozi wa CCM. Alisema kitendo cha kuingiza chama katika mambo yake binafsi kimemsikitisha, hivyo na yeye hatavumilia hayo.

Alisema si yeye tu anayemiliki ardhi katika kijiji hicho, kwani hata Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa (Waziri Mkuu mstaafu) ana ekari za kutosha katika eneo hilo pamoja na diwani wa Monduli Juu na wengine walioko ndani ya Chadema.

Lakini, alisema hao wote hawakuguswa, kwa sababu ni wana Chadema.

Alidai huo ni ubaguzi na uchochezi na unapaswa kupigwa vita. Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Monduli, Amani Ole Silanga, aliwataka wanakijiji kuwa na subira, kwani huo ni upepo mchafu unaovuma kupitia baadhi ya viongozi wa halmashauri na baraza la madiwani.

Alisisitiza kuwa upepo huo mchafu utapita. Laigwanani, Oleleku Ndeese aliitaka CCM kusimamia hilo kwani Chadema iko Monduli kutaka kupora haki za watu na hilo halitavumilika kamwe na ameomba wasaidie damu isimwagike.

Morani, Songoro Matata alihamasisha wanakijiji walioko kwenye vyama vya siasa kupima na kuona ni chama gani kipo kutetea maslahi ya wananchi na kukifuata chama hicho.

Hivi karibuni Baraza la madiwani la Halmashauri ya wilaya ya Monduli, lilipitisha azimio la kuchukua ardhi ya kijiji hicho kwa madai kuwa waliochukua ardhi hiyo hawakufuata sheria, akiwemo mwenyekiti wa CCM wa wilaya hiyo.