SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Alhamisi, 29 Juni 2017

T media news

Taarifa Muhmu Toka Ofisi ya Makamu wa Rais

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassan amewaagiza wapelelezi na waendesha mashtaka nchini waepukane na vitendo vya rushwa bali wafanye kazi kwa bidii kwa kuweka maslahi ya Taifa mbele kwa kuchukua hatua stahiki kwa watu wanaoiba rasilimali za Taifa.

Makamu wa Rais ametoa kauli hiyo wakati anazindua mwongozo kwa wapelelezi na waendesha mashtaka wa kesi za wanyamapori na misitu katika ukumbi wa Kimataifa wa Julius Kambarage Nyerere jijini Dar es Salaam.

Makamu wa Rais amesema mwongozo aliouzindua utasaidia kwa kiwango kikubwa uboreshwaji wa upelelezi na uendeshaji wa kesi zinazohusu wanyapori na misitu nchini.

“Uwepo wa mwongozo huu ni dhahiri unategemewa kutoa matokeo chanya katika mapambano dhidi ya ujangili na uharibifu wa misitu yetu,” amesisitiza Makamu wa Rais.

Makamu wa Rais amesema kuwa ana imani mwongozo huo aliouzindua utasaidia kukomesha vitendo vya uhalifu ambavyo vimekuwa vikiisababishia Serikali hasara kubwa ikiwemo uharibifu wa rasilimali za Taifa na kupoteza mapato ambayo yangesaidia kuimarisha huduma za kijamii nchini.

Kuhusu sekta ya utalii nchini, Makamu wa Rais amesema pamoja na sekta hiyo kuliingizia Taifa mapato mazuri lakini inasikitisha kuona kuwa uwepo wa wanyamapori ambao ndio nguzo kuu ya sekta ya utalii unazidi kupungua kila kukicha hivyo kuwa tishio kubwa kwa uchumi na nchi.

Amesema vitendo vya ujangili vimeendelea kuangamiza wanyama hasa tembo, hivyo ni muhimu kwa wapelelezi na waendesha mashtaka kutenda haki bila kuonea mtu kwa watu wanaokamatwa kufanya vitendo hivyo ili viweze kukomeshwa nchini.

“Wazee wetu walilinda na kutunza rasilimali zetu kwa faida yetu nasi tuzitunze kwa ajili ya vizazi vijavyo,”ameeleza.

Kwa upande wake, Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe amemhakikishia Makamu wa Rais kuwa kazi ya kupambana na ujangili na utoroshaji wa wanyama na viumbe wengine itakuwa endelevu na wale wote  watakaokamatwa watachukuliwa hatua kali za kisheria ili kukomesha vitendo hivyo.

Waziri Profesa Maghembe amemwomba Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini kuendesha operesheni maalum ya kukusanya silaha zote ambazo zimekuwa zikitumika kwenye ujangili ili kuhakikisha wanyama hasa tembo wanakuwa salama kwenye maeneo ya Hifadhi za Taifa nchini.

Naye, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali Biswalo Mganga amefafanua kuwa katika kipindi cha mwaka 2014-2017 ofisi yake imewafikisha Mahakamani washtakiwa wakubwa wa ujangili ambao walihukumiwa vifungo virefu na faini.

Amesema kuwa washtakiwa 100 walihukumiwa kulipa faini ya zaidi ya shilingi bilioni 1.1 kwa kujihusisha na nyara za Serikali kinyume na sheria na faini hizo zimeshalipwa Serikalini.

Ameeleza kuwa kati ya idadi hiyo watuhumiwa zaidi ya 80 walihukumiwa kifungo cha miaka 20 hadi 30 gerezani na faini ya zaidi ya shilingi milioni 164 ambazo bado hazijalipwa Serikalini.

Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali Biswalo Mganga amesema mafanikio hayo yote yamechangiwa na usimamizi madhubuti wa kesi hizo kupitia dawati la wanyamapori katika Divisheni ya Mashtaka pamoja na Mawakili wa Serikali katika Ofisi zote za mikoani nchini.

Ameeleza kuwa changamoto kubwa wanayokutana nayo kwenye kazi kwa sasa ni dhamana kwa watuhumiwa wakubwa wa vitendo vya ujangili ambapo utafiti uliofanywa Mahakama za mkoa wa Dar es salaam tu katika kipindi cha mwaka 2010 hadi 2015 unaonyesha kuwapo kwa jumla ya mashauri 13 yanayohusishwa na nyara za Serikali zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 800 zilizokamatwa ndani na nje ya nchi ambapo watuhumiwa wake walipewa dhamana na kutoweka.

Biswalo Mganga amesema katika mashauri hayo, asilimia 69 walikuwa ni raia wa kigeni na asilimia 31 ni raia wa Tanzania.

Imetolewa na

Ofisi ya Makamu wa Rais wa

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ikulu – Dar es Salaam.