Chama cha Mapinduzi (CCM) kimepinga vikali kauli iliyotolewa na mwanasiasa mkongwe hapa nchini kuhusu Masheikh wa Uamsho kikisema kuwa kauli hiyo ni ya kidi ni na kichochezi.
Chama hicho kimeitaka serikali kutofumbia macho watu wa hivyo na kwamba endapo watathibitisha kuwa kauli hiyo haikuwa na mrengo mzuri katika jamii, wasisite kumchukulia hatua mhusika mkuu.
Akizungumza leo na waandishi wa habari, Humphrey Polepole ambaye ni Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, alisema chama hicho kinalaani kauli iliyotolewa na Lowassa katika futari aliyokuwa amealikwa.
Katika futari hiyo, Lowassa aliwataka waislamu nchini kutokuwa wa baridi wakaishia tu kuongea badala yake watafute lugha nyingine ambayo wakizungumza serikali itaielewa ili viongozi wa dini hiyo wanaoshikiliwa kwa miaka minne sasa waweze kuachiwa.
Kufuatia kauli hiyo ambayo Polisi walisema kuwa ni ya kichochezi, Lowassa aliitwa na tayari kuhojiwa na Polisi siku ya Jumanne na alitakiwa kurudi tena leo. Alipokwenda leo mahojiano hayo yalishindakana kufanyika kwa madai kuwa upelelezi dhidi yake haujakamalika na hivyo kutakiwa kurejea Julai 13.
Katika hatua nyingine, Polepole amesema kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinaunga Mkono Kauli ya Rais Magufuli ya kutorudi masomoni kwa wanafunzi waliopata ujauzito wakiwa shule kwenye mfumo rasmi wa Elimu.
Polepole amesema kuwa wanafunzi waliopata ujauzito hawataweza kurudi shuleni kwenye mfumo rasmi isipokuwa kwenye Mfumo wa elimu ya watu wazima.