SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Alhamisi, 29 Juni 2017

T media news

Rais Mgufuli Akutana na Wataalam Wa Umeme Ehiopia .......Wazungumzia Uzalishaji wa Megawati 2, 100 za Umeme katika Maporomoko ya mto Rufiji

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli  jana  tarehe 28 Juni, 2017 amekutana na timu ya wataalamu wa masuala ya umeme na ujenzi wa mabwawa ya maji ya kuzalisha umeme iliyotumwa na Waziri Mkuu wa Ethiopia Mhe. Hailemariam Desalegn kwa lengo la kubadilishana uzoefu na Tanzania.

Mhe. Rais Magufuli alisema timu hiyo inayoongozwa na Waziri wa Maji, Umwagiliaji na Umeme wa Ethiopia Dkt. Seleshi Bekele imekuja nchini kubadilishana uzoefu na timu ya wataalamu wa Tanzania ambayo inasimamia utekelezaji wa ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme katika maporomoko ya mto Rufiji (Stiegler’s Gorge Power Project).

Katika mazungumzo na timu hiyo yaliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam, Mhe. Rais Magufuli alielezea nia yake ya kuhakikisha mawazo ya Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere ya tangu mwaka 1980 juu ya kuzalisha umeme kutoka maporomoko ya mto Rufiji, yanatekelezwa haraka iwezekanavyo.

“Sasa hivi nchi yetu inazalisha megawatts 1,450 tu, lakini Stiegler’s Gorge itatuzalishia megawatts 2,100 umeme huo ni mwingi na utatusaidia katika viwanda, hivyo Serikali tumeamua kutekeleza mradi huu.

“Najua kutaanza kutokea vipingamizi mbalimbali, lakini naomba Watanzania tuwe na sauti moja, eneo litakalotumia ni Kilometa za mraba 1,350 ambalo ni sawa na asilimia 3 tu ya eneo lote la hifadhi ya Selous yenye ukubwa wa Kilometa za mraba 45,000” alisema Mhe. Rais Magufuli na kuongeza kuwa mradi huo utakuwa na faida nyingi zikiwemo uvuvi, maji kwa ajili ya wanyamapori na kilimo.

Kwa upande wake Waziri wa Maji, Umwagiliaji na Umeme wa Ethiopia Dkt. Seleshi Bekele alisema Ethiopia ambayo kwa sasa inazalisha megawatts 4,300 za umeme kwa kutumia maji, inayo miradi mingi ya kuzalisha umeme kwa kutumia maji ambayo itaiwezesha kufikia uzalishaji wa megawatts 17,000 ifikapo mwaka 2020 na kwamba yeye na watalaamu wa nchi wapo tayari kubadilishana uzoefu na Tanzania katika masuala ya umeme na ujenzi wa mabwawa ya maji ya kuzalisha umeme.

Mazungumzo hayo yalihudhuriwa na Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi John Kijazi, Naibu Waziri wa Nishati na Madini wa Tanzania Dkt. Medard Kalemani na timu ya wataalamu wa Tanzania wanaosimamia utekelezaji wa ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maporomoko ya mto Rufiji (Stiegler’s Gorge Power Project).