Atiwa mbaroni Algeria kwa mashambulio ya Paris

Maafisa usalama wa Algeria wametangaza habari ya kutiwa mbaroni raia mmoja wa nchi hiyo aliyekuwa anaishi nchini Ubelgiji kwa tuhuma za kuhusika katika mashambulizi ya mjini Paris Ufaransa.Shirika la habari la Algeria limetangaza leo Jumapili kuwa, mtuhumiwa huyo ambaye alitiwa mbaroni Jumanne iliyopita, alikamatwa mashariki mwa Algeria.Hata hivyo mwendesha mashtaka mkuu wa Algeria hakutoa wasifu wa mtuhumiwa huyo, lakini amesema, ametiwa mbaroni kwa kuhusika na shambulio la kigaidi la mwezi Novemba mwaka jana mjini Paris na kuwa na uhusiano na kundi moja la kigaidi lililoko nje ya Algeria.Kwa upande wake, gazeti la Le Soir la Algeria limelinukuu shirika la habari la Ufaransa likisema kuwa, mtuhumiwa huyo anajulikana kwa jina la Zahir Mahdawi mwenye umri wa miaka 26 ambaye aliondoka Algeria mwaka 2012 na kuelekea nchini Uturuki.Itakumbukwa kuwa, watu 130 waliuawa na mamia ya wengine kujeruhiwa baada ya watu wenye silaha kufanya mashambulizi katika maeneo tofauti ya Paris, mji mkuu wa Ufaransa, tarehe 13 Novemba, 2015.