Mshauri wa Rais wa Syria amesema kuwa kundi la kigaidi la ISIS au Daesh linaweza kuangamizwa haraka iwapo baadhi ya nchi za eneo hasa Uturuki na Saudi Arabia zitaacha kuliunga mkono kifedha na kisiasa kundi hilo la wakufurishaji.Katika mahojiano na Televisheni ya RT, Bi. Bouthaina Shaaban amesema magaidi wanaopata himaya ya kigeni ni kizingiti kikuu katika kumaliza mgogoro nchini humo.Mshauri huyo wa Rais Bashar al Assad pia amezikosoa nchi za Magharibi na hasa Marekani kwa kuunga mkono kisiasa kundi la ISIS.Akigusia mazungumzo ya amani baina ya serikali ya Syria na kile kinachotajwa kuwa ni upinzani, amesema mazungumzo hayo hayajaweza kufanyika kwa sababu makundi ya upinzani yanaungwa mkono kifedha na nchi mbali mbali. Amesema upinzani nchini Syria ni upinzani pekee duniani ambao ni kibaraka wa madola ya kigeni dhidi ya nchi yao.Buthaina Shaaban ameelezea matumaini yake kuwa usitishwaji vita nchini Syria unaoanza siku ya Jumamosi utafanikisha kufikiwa umoja wa kitaifa na kuongeza kuwa Wasyria wamepigana miaka mitano ili kuhakikisha nchi yao haigawanywi vipande vipande.Katika kipindi cha karibu miaka mitano ya hujuma za magaidi Syria, takribani watu 470,000 wamepoteza maisha na mamilioni ya wengine kuachwa bila makazi.