SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Ijumaa, 26 Februari 2016

T media news

Chenge ajigamba fundi wa kutengeneza fitina




Mbunge wa Bariadi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge   

Bariadi. Mbunge wa Bariadi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge amesema kuwa yeye ni fundi wa kutengeneza fitina kwa watumishi wasiokuwa waadilifu.

Chenge alisema hayo juzi katika kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi walipokuwa wakijadili na kupitisha rasimu ya bajeti ya mwaka ujao wa fedha 2016/2017 mjini hapa.

Alisema mtendaji yeyote asiye muadilifu ni bora aombe kuhama kabla hajamshukia kama mwewe.

Alisema hatakubali kuona wananchi wakiendelea kuibiwa na kunyanyaswa wanapokwenda kupata huduma katika ofisi za umma.

“Hatujaruhusu mtu yeyote aje Bariadi kufanya kazi kwa ajili ya kuwaibia wananchi, mimi ni fundi wa fitina, nitafanya kila linalowezekana ili niwaondoe haraka watu wa aina hii,” alisema Chenge.

Alisema hakuna sababu ya kuacha wananchi waendelee kunyanyasika wakati watumishi wa Serikali na wanasiasa wilayani humo kwa pamoja wanajenga nyumba moja ambayo ni Bariadi.

Katika hatua nyingine, Chenge aliwataka madiwani kumpa ushirikiano Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Abdallah Malela kwa kuwa anasimamia miradi mingi ya maendeleo katika halmashauri yao.

Akizungumza kwenye kikao hicho, Diwani wa kata ya Gilya, Lewa Safari alisema kuna baadhi ya askari wanyamapori wanawanyanyasa wananchi wanaoishi jirani na hifadhi zilizoko wilayani humo kwa kuwalazimisha kuwapa fedha ili wawaachie walishe mifugo yao.

Lewa alisema hali hiyo inawaweka katika wakati mgumu wananchi hasa wale wa kipato cha chini.    

 6  0 0  0  0