Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema anatiwa wasiwasi na kutiwa nguvuni baadhi ya wapinzani wa kisiasa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na mbinyo wa kisiasa unaoshuhudiwa nchini humo.Idadi kadhaa ya wanaharakati wa kisiasa wa eneo la mashariki mwa Kongo DR wamehukumiwa kifungo cha maisha jela kwa tuhuma za kuchochea uasi dhidi ya serikali. Aidha Mahakama Kuu ya mji wa Goma ulioko kwenye mpaka wa mashariki wa nchi hiyo imewahukumu adhabu ya kifungo cha miaka miwili jela wanaharakati sita wa Harakati ya Wananchi ya Mapambano kwa ajili ya Mabadiliko.Ilidaiwa mahakamani na upande wa serikali ya Kinshasa kuwa watu hao ni waasi. Itakumbukwa kuwa wapinzani na wanaharakati wa asasi za kiraia nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo walitoa wito kwa wananchi kushiriki kwenye maandamano ya kupinga serikali ambayo yalikuwa yamepangwa kufanyika tarehe 16 ya mwezi huu wa Februari katika mji mkuu wa nchi hiyo Kinshasa.Tarehe 16 Februari, inaadhimishwa kukumbuka umwagaji damu wa mwaka 1992 uliofanywa na utawala wa aliyekuwa dikteta wa nchi hiyo Mobutu Sese Seko dhidi ya wananchi walioandamana katika mji mkuu Kinshasha kwa lengo la kuuangusha utawala wake wa kiimla. Wadadisi wa mambo wanasema, kutolewa wito na wapinzani wa kisiasa wa Kongo DR kwa wananchi kushiriki kwenye maandamano katika siku ya maadhimisho ya kukumbuka ukandamizaji wa umwagaji damu uliofanywa na utawala wa Mobutu, ni ishara ya kushadidi upinzani dhidi ya kuendelea kubakia madarakani Rais Joseph Kabila wa nchi hiyo.Kabila ambaye amekusudia kugombea tena urais kwa muhula wa tatu mfululizo anakabiliwa na upinzani wa vyama vya siasa na asasi za kiraia dhidi ya mpango wake huo. Kwa mujibu wa Katiba, uchaguzi mkuu umepangwa kufanyika mwezi Novemba mwaka huu.Hata hivyo viongozi wa chama tawala cha Wananchi kwa ajili ya Ujenzi Mpya na Demokrasia (PPRD) ambao wanataka Kabila aendelee kubakia madarakani wanataka kutumia kisingizio cha uhaba wa fedha za bajeti ya uchaguzi ili kusogeza mbele tarehe ya kufanyika uchaguzi huo. Kwa mtazamo wa wakosoaji, kusogeza mbele tarehe ya uchaguzi wa rais na bunge ni silaha inayotumiwa ili kurefusha muda wa utawala wa Rais Joseph Kabila. Na hii ni katika hali ambayo kwa mtazamo wa vyama vya upinzani kiongozi huyo alishinda katika uchaguzi wa rais wa mwaka 2011 kwa udanganyifu na kwa kueneza wimbi la hofu na vitisho nchini humo. Joseph Kabila amekuweko madarakani tangu alipouliwa baba yake Laurent Desire Kabila mwezi Januari mwaka 2001. Alishinda katika chaguzi zilizofanyika mwaka 2006 na 2011 kwa kupata takribani asilimia 60 ya kura. Hata hivyo wagombea urais wa vyama vya upinzani hususan mwanasiasa mkongwe wa nchi hiyo Étienne Tshisekedi hakukubali kuyatambua matokeo ya uchaguzi huo. Tarehe 20 Desemba miaka mitano iliyopita, sambamba na Kabila kula kiapo cha urais, Tshisekedi alijitangaza rais halali wa Kongo DR. Hata hivyo upinzani wa mwanasiasa huyo haukusaidia kitu zaidi ya kuishia kutiwa nguvuni na kuwekwa ndani kwa muda kisha kuachiliwa huru.Baada ya kuhudumu vipindi viwili vya urais na licha ya kukabiliwa na malalamiko ya wapinzani na ya harakati za wananchi za kuunga mkono demokrasia, Kabila ameonyesha wazi kuwa ana nia ya kuwania tena urais kwa muhula wa tatu.Kuakhirisha uchaguzi kunaonekana kama mbinu na hila ya kuwanyamazisha wapinzani wa kiongozi huyo ili kwa njia hiyo au kwa kutumia silaha nyengine kuwafanya wakubaliane na mpango wake wa kutaka aendelee kubakia madarakani.Kuendelea kubakia madarakani kwa kubadilisha baadhi ya vifungu vya Katiba, hivi sasa umekuwa ndio mtindo wa viongozi wengi wa nchi za Kiafrika. Lakini inavyoonekana, Kabila na waitifaki wake katika chama tawala cha PPRD wamekusudia kutumia njia za amani na za kidemokrasia zaidi ili kufikia lengo hilo.Hayo yanajri katika hali ambayo kutiwa nguvuni na kufungwa jela baadhi ya wapinzani kumemtia wasiwasi Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa pamoja na jumuiya nyengine za kimataifa. Ukandamizaji wa kisiasa ni matokeo ya ukiritimba wa kuhodhi madaraka unaofanywa na watawala madikteta ambao wananchi wa mataifa mengi ya Afrika waliushuhudia katika miaka ya muongo wa 1990 chini ya tawala za chama kimoja cha siasa au za kijeshi. Hivi sasa hali inayofanana na hiyo inashuhudiwa nchini Burundi. Inavyoonekana, wasiwasi alioonyesha kuwa nao Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa juu ya anga ya mbinyo wa kisiasa inayotawala Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo hautoshi. Wananchi wa nchi hiyo na wa nchi nyengine za Kiafrika ambao viongozi wao wamesibiwa na ugonjwa wa uchu wa madaraka wana matarajio ya kuuona Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa zikichukua hatua za lazima na za maana kukabiliana na hali hiyo.../