Mkali wa bongo fleva kutoka Kundi la TMK Wanaume Family lenye maskani yake Temeke Dar es Salaam Chege Chigunda, amevunja ukimya kuhusu uhai wa kundi hilo na kusema kuwa kundi hilo halijafa isipokuwa hawakuwa na mpango wa kutoa ngoma mwaka huu.
Kundi hilo ambalo liko chini ya usimamizi wa Mkubwa Fella limekuwa kimya tangu mwaka huu uanze.
eNewz ilizungumza na mmoja kati ya wasanii wanaounda kundi hilo Chegge na alisema kuwa kundi hilo halijafa na kwamba wanachoangalia wao ni soko la muziki linaendaje na siyo kwamba mwaka umeisha bila wao kutoa ngoma.
“Kundi la TMK lipo sana na siyo kwamba limekufa kama watu wanavyodai na pia sisi tuanaangalia soko linaendaje na siyo vinginevyo kama tukiona kwa sasa soko la muziki halijakaa poa basi na sisi hatutoi ngoma, kama umeona hata mimi na Temba kwa sasa hatujatoa ngoma hata moja tuko kimya tu hiyo yote ni kwa sababu ya soko lilivyo kwa sasa “
Chege na Temba ni moja kati ya wasanii katika kundi hilo ambalo kwa mwaka huu mzima hawajafanikiwa kutoa ngoma hata moja.