SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatatu, 29 Agosti 2016

T media news

BREAKIN NEWZZ!!:- HATIMAYE MAALIM SEIF HAMADI AIZIKA CUF UPANDE WA BARA SOMA HAPA LIVE!!

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Imetolewa leo tarehe29/8/2016

 
Ndugu Waandishi wa habari,
Awali ya yote naomba nianze kwa kumshukuru
Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia uhai na uzima
wa afya na tukaweza kukutana hapa asubuhi hii
ya leo. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu pia kwa
kuijaalia nchi yetu kuendelea kubaki katika hali
ya amani na utulivu licha ya matatizo mengi
yanayotukabili.
 
Pili, nichukue fursa hii kukushukuruni nyinyi
waandishi wa habari kwa kuitikia wito wetu na
kuja kutusikiliza. Ni imani yangu kuwa kama
ambavyo mmekuwa mkitupa mashirikiano
mazuri katika kuwafikishia wananchi yale
ambayo chama chetu kupitia kwenu kimekuwa
kikiyatolea taarifa, kwa uzito wa kipekee taarifa
hii nayo mtawafikishia Watanzania wote kupitia
vyombo vyenu vya habari.
Ndugu Waandishi wa habari,
 
Tumewaita leo hii kuwaeleza juu ya maazimio ya
kikao cha Baraza Kuu la Uongozi la Taifa katika
kikao chake cha dharua kilichofanyika jana,
Jumapili ya tarehe 28/08/2016 Katika ukumbi wa
Makao Makuu ya Chama, ofisi za Vuga. Kikao
hicho kilichoongozwa na Mwenyekiti wa muda
Mhe, Hamidu Hassan Bobali, Mbunge wa Jimbo
la Mchinga kilihudhuriwa wa Wajumbe 46 katika
ya Wajumbe 60.
 
Ndugu Wandishi wa Habari,
 
Kama mnavyojua tarehe 21/08/2016 Chama Cha
Wananchi – CUF kilikuwa na Mkutano Mkuu
Maalum wa Taifa uliofanyika katika ukumbi wa
Blue Pearl, Ubungo Plaza, Dar es Salaam.
Mkutano huo ulikuwa na agenda mbili kuu,
ambazo ni:-
 
1. Kupokea barua ya Profesa Ibrahim Haruna
Lipumba ya kujiuzulu nafasi yake ya uenyekiti ya
tarehe 05/08/2015; na
2. Kufanya Uchaguzi wa kujaza nafasi zilizo wazi
- Mwenyekiti Taifa, Makamu Mwenyekiti na
Wajumbe wanne wa Baraza Kuu la Uongozi la
Taifa.
 
Kufuatia hujuma za makusudi zilizoandaliwa kwa
mashirikiano ya maadui wa ndani na nje ya
chama, aliyekuwa Mwenyekiti wa muda wa
Mkutano Mkuu Maalum, Mhe Julius Mtatiro
alilazimika kuakhirisha Mkutano ule mara baada
ya kumalizika kwa ajenda ya kwanza ambapo
Mkutano Mkuu uliridhia kujiuzulu kwa Profesa
Ibrahimu Haruna Lipumba kwa azimio lililoungwa
mkono na wajumbe 476 dhidi ya wajumbe 14
waliokataa. Hivyo basi agenda namba 2
haikuwahi kukamilishwa, na kwa hivyo
haikufanyiwa maamuzi.
 
Kikao cha Baraza Kuu la Uongozi, kilichokaa jana
kimejadili kwa kina juu ya hujuma za kuvuruga
Mkutano Mkuu Maalum wa tarehe 21/08/2016.
Baraza kuu limesikitishwa sana na kitendo kile
ambacho mbali ya kukisababishia chama hasara
ya zaidi ya Shillingi milioni 600, pia kimepelekea
kuharibu taswira ya chama ndani na nje ya nchi.
Baraza Kuu lilipata nafasi ya kupokea maelezo
ya kina kutoka kwa wajumbe mbali mbali hasa
wale wanaotokea Tanzania Bara walioeleza
kwamba hujuma zilizofanywa kuvuruga Mkutano
Mkuu Maalum wa Taifa wa tarehe 21 Agosti,
2016 hazikuwa za bahati mbaya au za
kushtukiza bali ni matokeo ya njama na mbinu
ovu na chafu ambazo zimekuwa zikipangwa na
kutekelezwa chini kwa chini kwa muda mrefu.
Wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa
walieleza kwa ushahidi jinsi baadhi ya viongozi
wa Chama walioaminiwa na kupewa nyadhifa za
juu walivyogeuka na kuanza kutumiwa na
maadui wa nje ya Chama kukihujumu Chama.
 
Baraza Kuu limezingatia kuwa CUF ni chama cha
kistaarabu, ni Chama cha Kidemokrasia na ni
Chama chenye kutoa matumini ya mabadiliko ya
kweli kwa Watanzania walio wengi. Vurugu
zilizojitokeza ni aibu na fedheha kwa chama
chetu mbele ya macho ya Watanzania na
wapenda demokrasia.
 
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa limeridhika
kwamba watu hao waliokuwa vinara wa vurugu
na njama hizo ovu walipewa nafasi mara kadhaa
kujirekebisha dhidi ya mwendo wao huo dhidi ya
Chama lakini waliendelea na vurugu na hujuma
zao hizo. Kwa hatua iliyofikia, Baraza Kuu
limeona halina njia nyengine ya kukinusuru
Chama isipokuwa kuchukua hatua kali na
madhubuti kukilinda Chama ambao ni wajibu
wake kikatiba.
 
Kwa msingi huu basi, Baraza Kuu la Uongozi la
Taifa kwa kauli moja (unanimously) limeamua
kuchukua hatua za kinidhamu kwa viongozi na
wanachama mbali mbali waliohusika kwa njia
moja au nyengine katika kuchochea vurugu zile.
Baraza kuu limechukua hatua mbili kubwa
ambazo ni kutoa karipio kali, kusimamisha na
kufukuza uanachama wahusika wote walioshiriki
kuchochea vurugu hizo.
 
Viongozi waliopewa karipio kali kwa mujibu wa
Katiba ya Chama, Ibara ya 83 (5)(b) ambao ni
wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa ni:
 
1. Rukiya Kassim Ahmed na
2. Athumani Henku
 
Viongozi waliosimamishwa uanachama kwa
mujibu wa Katiba ya Chama, Ibara ya 83 (5)(c),
hadi hapo watakapopata fursa ya kujieleza
mbele ya Baraza Kuu ni;
 
1. Prof Ibrahim Haruna Lipumba
2. Magdalena Sakaya
3. Abdul Kambaya
4. Ashura Mustafa
5. Omar Mhina Masoud
6. Thomas Malima
7. Kapasha M. Kapasha
8. Maftaha Nachumu
9.Mohamed Habib Mnyaa
10. Haroub Shamis
na
11. Mussa Haji Kombo
 
Mwanachama aliyefukuzwa chama ambaye
alipata fursa ya kujieleza mbele ya Baraza Kuu
na kikao kuamua kumfukuza chama kwa mujibu
wa Katiba ya Chama, Ibara ya 83 (5)(c) ni
aliyekuwa Kaimu Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya
Wazee wa CUF (JUWACUF), Shashu Lugeye.
Kufuatia maamuzi hayo, Baraza Kuu la Uongozi
la Taifa limewateua viongozi mbali mbali
kukaimu nafasi mbali mbali zilizoachwa wazi.
Kwa kuzingatia kwamba kutokamilika kwa
Mkutano Mkuu Maalum wa Taifa wa tarehe 21
Agosti, 2016 kulipelekea kushindwa kufanyika
kwa uchaguzi wa Mwenyekiti na Makamu
Mwenyekiti wa Chama, Baraza Kuu la Uongozi la
Taifa limetumia uwezo liliopewa na Katiba ya
Chama, Ibara ya 101 na 118, kuunda Kamati ya
Uongozi ambayo itakuwa ikifanya kazi za
Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti hadi hapo
uchaguzi wa kujaza nafasi hizo utakapofanyika.
 
Baraza Kuu la Uongozi limewateua wafuatao
kuwa wajumbe wa Kamati hiyo ya Uongozi:
 
1. Mhe. Julius Mtatiro – Mwenyekiti;
2. Mhe. Katani Ahmed Katani – Mjumbe; na
3. Mhe. Severina Mwijage – Mjumbe.
 
Aidha Baraza Kuu la Uongozi la Taifa, kwa
kufuata Ibara ya 105 (1) na (3) ya Katiba ya
Chama, limemteua Mhe. Joran Bashange kuwa
Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa Chama kwa
upande wa Tanzania Bara na Mhe. Mbarala
Maharagande kuwa Kaimu Naibu Mkurugenzi wa
Habari, Uenezi na Mawasiliano kwa Umma hadi
hapo nafasi hizo zitakapojazwa rasmi kwa
mujibu wa masharti ya Katiba ya Chama.
 
Mwisho, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa
linawahakikishia wanachama na wapenzi wake
na Watanzania wote kwa ujumla kuwa Chama
Cha Wananchi – CUF kipo imara na makini na
katu hakitoyumbishwa kwa hila na njama ovu na
chafu zinazofanywa na maadui wa chama hichi.
Tangu kuasisiwa kwake, CUF imeandamwa na
maadui wa kila aina, na imepitia katika misuko
suko mingi. Tunaamini hila na njama hizo ovu
zimekuwa zikielekezwa CUF kwa kutambua
kwamba Chama hichi ndicho kinachobeba
dhamira ya dhati ya kuleta mabadiliko ya kweli
hapa nchini.
 
Kutokana na umadhubuti, umakini na uimara wa
Katiba ya Chama na safu ya viongozi wake, CUF
imeweza kuvuka salama kila ilipoingia katika
misuko suko hiyo na kwa hivyo, hata wimbi hili
lililoonekana kukitikisa Chama limekabiliwa
ipasavyo na sasa kazi iliyopo mbele yetu ni
kuendeleza harakati za kisiasa za kuwaletea
Watanzania wa Bara na Zanzibar mabadiliko
wanayoyataka.
 
HAKI SAWA KWA WOTE
Nassor Ahmed Mazrui- +255 777 426 975
NAIBU KATIBU MKUU CUF
 
Mawasiliano: Mkurugenzi Habari - Salim Biman
077414112
 
K/Naibu Mkurugenzi : Mbarala Maharagande-
0784 001408