Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kesho linaanza shamrashamra za maandalizi kuelekea siku ya maadhimisho ya 52 ya majeshi inayotarajiwa kufanyika Septemba Mosi mwaka huu kwa kufanya usafi na upandaji miti katika kambi za jeshi na baadhi ya taasisi nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam, Msemaji wa JWTZ Kanali Ngemela Lubinga amewatoa hofu wananchi kuwa wasitishike pindi watakapoona wanajeshi katika maeneo ya karibu na makazi yao.
“Kesho tuaanza kufanya usafi kuanzia maeneo ya Kawe hadi karibu na kambi ya Lugalo, na kwamba niwatoe hofu wananchi pindi watakapoona wanajeshi wengi mitaani kwa kuwa hatuna nia mbaya hivyo wasitufikilie vibaya,” amesema.
Amesema jeshi hilo litafanya usafi pamoja na upandaji miti katika baadhi ya maeneo nchini hadi siku ya kilele cha maadhimisho hayo. Pia wanajeshi watajitolea damu salama katika hospitali za kambi za jeshi.
“Siku kuu ya majeshi itaadhimishwa pamoja na wanajeshi kujitolea damu kwenye vituo maalumu vya kutolea damu salama mikoani, katika hospitali zetu za kanda,” amesema na kuongeza.
“Sanjari na utoaji damu, madaktari wetu JWTZ watatoa huduma za tiba bure kama upimaji wa virusi vya Ukimwi, kisukari, na upimaji wa shinikizo la damu. “
“Kama ilivyo mila na desturi ya majeshi kufanya usafi na utunzaji wa mazingira, kuelekea siku ya maadhimisho tutafanya usafi na kupanda miti maeneo ya jirani na kambi na kwenye taasisi za kiraia kadri mahusiano yatakavyofanyika na taasisi hizo, ” amesema.
Pia amesema siku hiyo ya maadhimisho itaadhimishwa kwa kuienzi michezo na kudumisha urafiki baina ya JWTZ, wananchi, na Taasisi na kwamba mashindano mbalimbali yatafanyika.