SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatatu, 2 Mei 2016

T media news

Waziri Makamba Awasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Serikali inaendelea kusimamia mazingira na kuhakikisha mifuko ya plastiki inayotumika nchini iwe ni ile inayokidhi viwango vianavyokubalika ili kuondokana na changamoto ya kuzagaa kwa mifuko hiyo katika maeneo mbalimbali. 

Kauli hiyo imetolewa leo Bungeni mjini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira na Muungano January Makamba alipokuwa akitoa hoja ya wizara yake kuidhinishiwa maombi ya fedha kwa mwaka wa fedha 2016/2017. 

Makamba amesema kuwa sababu kubwa ya kusambaa kwa mifuko ya plastiki inatokana na mifuko hiyo kutolewa bure na hivyo kuchafua mandhari na kuziba mifereji sehemu mbalimbali hali inayosababisha athari kubwa katika mazingira. 

“Asilimia kubwa kwenye mito, maziwa na fukwe za bahari imejaa mifuko ya plastiki, hali hii ni hari kwa usalama wa mazingira yetu” alisema Makamba. 

Akiwasilisha hotuba yake, Waziri Makamba amesisitiza kuwa mifuko ya plastiki isiyotakiwa kutumika nchini ni ile yenye unene chini ya maikroni 50 ambayo hairuhusiwi kuzalishwa wala kuingizwa. 

Kwa mujibu wa maelekezo ya bajeti ya mwaka wa fedha 2015/2016, Waziri huyo amesema kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais imekamilisha kanuni mpya ya mifuko ya plastiki zinazorekebisha viwango vya unene unaoruhusiwa kutoka Maikroni 30 kwenda Maikroni 50. 

Waziri Makamba amesema kuwa kanuni hizo tayari zimesainiwa kupitia tangazo la Serikali Na.271 la mwaka 2015 na kutolewa katika Gazeti la Serikali Julai 17, 2015 na kupewa Na. 29.