Saudia yatishia kutumia nguvu za kijeshi kumuondoa Rais wa Syria madarakani
Saudi Arabia imerudia kauli zake za kifedhuli za kuingilia masuala ya ndani ya Syria kwa kutishia kwamba endapo mazungumzo ya kisiasa ya kutatua mgogoro wa nchi hiyo yatafeli itatumia nguvu za kijeshi dhidi ya Rais Bashar al-Asaad.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudia Adel al-Jubeir baada ya mazungumzo ya Kundi la Kimataifa la Kuiunga Mkono Syria (ISSG) yaliyofanyika jana mjini Vienna, Austria.
Al-Jubeir amedai kuwa anavyoamini ilipasa muda mrefu nyuma kufikiria mpango mbadala, ambao unatilia nguvu kuwapatia misaada zaidi ya kijeshi wapinzani wa Rais Bashar al-Assad wa Syria.
Utawala wa Aal Saudi ni miongoni wa waungaji mkono wakubwa wa mpango wa kumwondoa madarakani Rais Assad na ni mfadhili mkubwa wa fedha na silaha kwa makundi yanayobeba silaha yanayotaka kuiangusha serikali halali ya Syria.
Duru ya mazungmzo yasiyo ya ana kwa ana ya kusaka amani baina ya serikali na wapinzani wa Syria yanayofanyika kwa usuluhishi wa Umoja wa Mataifa, yaliyoanza tarehe 13 ya mwezi uliopita mjini Geneva, Uswisi yalisita baada ya kundi la upinzani linaloungwa mkono na Saudia linalojiita Kamati ya Juu ya Mazungumzo (HNC) kujiondoa kwenye majadiliano na kutangaza "vita vipya" dhidi ya serikali ya Syria.
Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Syria Staffan de Mistura amekadiria kuwa watu zaidi ya laki nne wameuawa katika vita na machafuko nchini Syria na kusababisha pia zaidi ya nusu ya watu wa nchi hiyo kubaki bila ya makazi, ambao idadia yao kabla ya kuanza vita ilikuwa karibu watu milioni 23.../
Maoni
Chapisha Maoni