NINI ESPERANÇA HATA WANGELETWA MAZEMBE, YANGA HII INAENDA HATUA YA MAKUNDI!!
Na Eusebius Paul
Mara ya mwisho kwa club ya Tanzania kufuzu hatua ya makundi ya michuano barani Africa ilikuwa mnamo mwaka 2003! Kipindi ambacho serikali ya awamu ya tatu ilikuwa chini ya utawala wa Benjamin ‘Che’ Mkapa, Daz Nundaz na hit song ya Kamanda ndiyo uliikuwa ‘wimbo wa taifa’ wakati huo; CR7 alikuwa bado anakimbiakimbia kwenye nyasi za Estádio José Alvalade akiwa na jezi Sporting Lisbon.
Kikosi kilichowajumisha wataalamu Juma Kaseja, Victor Costa Nampoka ‘Nyumba’, Boniface Pawasa, Mrundi Ramadhan Wasso, Christopher Alex ‘Masai’ (R.I.P), Selemani Matola (captain), Shekhan Rashid, Ulimboka Mwakingwe ‘Uli’, Yusuph Macho ‘Musso’, Emmanuel Gabriel ‘Batistuta’, Joseph Kaniki ‘Golota’ na Steven Mapunda ‘Garrincha’ chini ya benchi la marehemu James Aggrey Siang’a kiliwashtua wengi barani Africa. Kipindi hicho mwandishi wa makala hii nikiwa darasa la 5B nikikariri kanuni ya MAGAZIJUTO pale Ligula Primary!
Zaidi ya kalenda 13 zimetundikwa na kutolewa ndani ya kuta za sebule zetu pasipo club yoyote iliyomudu kufikia hatua hiyo ya kujivunia. Lakini hatimaye ni Yanga hii yenye kikosi timamu na yenye uwezo wa kuleta maangamizi dhidi ya mpinzani yeyote, yenye uwezo wa kulirejesha tena Taifa hili katika hatua hiyo yenye heshima kila kona ya bara hili.
Hatua waliyopiga Yanga na ubora wao mpaka sasa
Baada ya kutembeza vichapo vya jumla ya mabao 3-0 dhidi Cercles de Joachim, na kuivurumisha APR ya Rwanda kwa mabao 3-2, mabingwa hao watetezi wa ligi kuu nchini walikwaana Al Ahly (Misri), na mabingwa hao wa kihistoria barani Africa kulazimika kusubiri mpaka dakika 94:52 kugusa wavu wa Yanga na hatimaye kuwazuia wanaume hawa ‘kwa shingo upande’.
Lakini kwa kutambua ugumu uliopo kufuzu hatua ambayo timu kama Yanga ilifikia na kwa muongozo wa kanuni za shirikisho la soka barani Africa (CAF) hatimaye Yanga ikasogea kutoka kwenye ligi ya Mabingwa na kuelekeza makali yake katika kombe la Shirikisho Africa. Mechi mbili za nyumbani na ugenini zikiamua nani atafuzu kuingia hatua ya nane bora kati ya Yanga dhidi ya wachimba madini waangola Esperança Sagrada.
Esperança Sagrada ndio nani?
Klabu hii inayomilikiwa na kampuni ya migodi ya almasi (Endiama) iliasisiwa rasmi mwaka 1976. Kuzaliwa kwa Espença ulikuwa ni sehemu ya mwitikio mkubwa kwa harakati za rais wa kwanza wa taifa hilo Agustinho Neto na utunzi wake wa shairi la ukombozi dhidi ya wareno ‘Sagrada Esperança’ (Matumaini matakatifu)! Historia yao katika mashindano ‘siyo mbaya’ ikiwa na mataji matatu ya michuano ya ndani na kufanikiwa kuiwakilisha Angola kimataifa mara saba. Na hatua ya mtoano waliyofikia msimu huu ndio mafanikio makubwa katika historia yao.
Tukirejea kwa upande wa wakilishi wetu Yanga, pamoja na maandalizi kabambe yanayohitajika ndani na nje ya uwanja ambayo naamini uongozi na benchi la ufundi vinayashughulikia, bado inapaswa kufanyia marekebisho kasoro kadhaa zilizojitokeza katika michezo yao takribani 38 mashindano mbalimbali msimu huu. Madhaifu makubwa yaliyoigharimu Yanga yamekuwa katika upande wa mipira ya kutenga (set pieces), mapambano ya mipira ya vichwa (aerial battles), kupoteza umakini katika dakika nyeti za kuamua mchezo(1-10 na 80-90) na mawasiliano ya katikati ya uwanja na waamuzi (communication with match officials).
Mosi, Set-pieces au mipira ya kutenga. Yanga imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara tano (5) katika mechi sita za kimataifa, na magoli matatu (60%) kati ya hayo yakitokana na mipira ya kona na faulo karibu na lango. Wachezaji wanatakiwa kuwa na umakini wa 101% pindi wanaporejea kulilinda lango nyakati za mapigo ya adhabu. Katika mechi ya Amahoro Stadium Rwanda, APR ilifunga goli baada ya golikipa kuponyokwa na mpira alioudaka. Kama kipa angeweka umakini na kupunguza mbwembwe za udakaji mpira usingemtoka mikononi katika harakati za kujidondosha, hali kadhalika mchezaji yule asingeweza kufunga iwapo mtu aliyepewa jukumu la kumkaba angestick naye mpaka kuhakikisha hakuna rapsha yoyote.
Katika mechi ya Dar dhidi ya Al ahly, mafarao walitumia trick ya kupigiana ‘faulo-pasi’ lakini mtu wa kwanza kufikiwa na ile pasi alikuwa hajakaa vizuri na kuamua kudonoa pasi ya kichwa kwenda angle ya pili ya goli. Pasi iliyomkuta mfungaji Amr Ghamaly akiwa peke yake na kuamua kuu-chip mpira kwenye nyavu za juu za Yanga wakati mabeki wote wakiwa wamejipanga kwenye mstari wa goli kulinda lango lao. Makosa yakaenda kujirudia mjini Cairo, mpira wa kona ulivyomiminwa ndani ya lango ulimkuta mfungaji aliyeruka kwa uhuru baada ya kumtoroka mkabaji wake. Mazoezi zaidi ya kukabiliana na mipira ya set-pieces yanahitajika.
Tatizo la pili ni mapambano ya mipira ya hewani (Aerial battles). Hatuwezi kukataa kuwa kimaumbile kuwa watu wengi wa ukanda wetu wa Mashariki tuna vimo vidogo kulinganisha na Africa Magharibi au Kaskazini. Lakini katika makosa yanayoigharimu Yanga hakuna hata moja lililokuwa nje ya uwezo wa wachezaji wetu. Mipira mingi ya hewani inayopotezwa inatoa mianya kwa wapinzani ku-force haraka kuja golini kwako sababu mara zote huinuliwa pindi team inapokaribia final third ya mpinzani.
Magoli yote matatu ya Al Ahly yalitokana na vichwa (2 headed goals, 1 headed assist), mechi ya Cairo itakuwa bado ipo vichwani mwa wengi. Goli la kwanza la Al Ahly wakati wa kona Hosam Ghaly alimtoroka yule fowadi wa Yanga aliyekuwa akimkaba na kwenda kupiga free header nyavuni, goli la pili mfungaji alitoka nje ya 18 kwa kasi na kwenda kukutana na krosi-dongo aliyoiunganisha kwa kichwa kizito na kufunga mbele ya beki aliyejaribu kuinua mguu kiuvivu ili aoshe mpira wa level ya kichwa. Mtaalamu Hans van Plujm anawajibu wa kuliwekea mkazo hili; Cannavaro, Tambwe, Ngoma na wenzao wasiwe tu wazuri wa kufunga kwa vichwa, bali wawe ‘waoshaji’ wazuri pia.
Tatizo la tatu, kupoteza umakini katika dakika nyeti za kuamua mchezo. Ukichunguza kwa makini magoli mengi msimu huu Yanga imefungwa katika dakika 10 za mwanzo au mwishoni mwa mchezo. Stand 81′, Mgambo 4′, Al ahly 90+5′, Al Ahly 10′, Kagera 6′, APR 90+1’…… Listi ni ndefu ya dakika za michezo ambayo Yanga imeruhusu nyavu zake kutikiswa. Inaonekana Yanga huanza mechi zake kwa kujivuta na mtindo wake kuanzia mashambulizi nyuma kati ya makipa na mabeki wao jambo lililosababisha wapinzani wao kuwapa pressure kubwa na hatimaye kufanya makosa yanayopelekea kufungwa mapema. Ilhali umakini mdogo dakika za lala salama zimefanya Yanga ifungwe magoli ya ‘usiku’.
Nne; Mawasiliano ya katikati ya uwanja baina ya wachezaji na waamuzi. Jukumu la mchezaji awapo uwanjani ni kucheza mpira na inapowezekana kupata muongozo kwa waamuzi ambao wana kazi za kutafsiri sheria. Lakini kuna nyakati nyingi za mchezo ambazo match official hufanya maamuzi tata kwa bahati mbaya ama kwa makusudio. Utashuhudia mara nyingi wachezaji wa timu za kigeni wakipata wasaa wa kuzungumza ‘hili na lile’ na waamuzi.
Mara kadhaa wachezaji wa Yanga chini ya nahodha Nadir haroub wamekuwa wazito kuelezea masahibu wanayokutana nayo iwe katika faulo za mfululizo, viwiko au upotezwaji muda hovyo. Mfano katika mechi ya Yanga vs Al Ahly ya Dar, Sherif Ekramy kipa wa waarabu alipoteza muda mwingi katika uanzishaji wa mipira lakini wachezaji walikuwa kimya ilhali uvumilivu ukiwaishia mashabiki jukwaani na kuanza zomeazomea iliyomlazimu mwamuzi Denis Dembele wa Ivori Coast kutoa kadi ya njano kwa kipa huyo kabla timu hazijaenda mapumziko.
Ajabu kipindi cha pili kabla ya kuanza kipa yule alienda kuzungumza na refa kwa takribani dakika mbili akimsihi hili na lile kishkaji, wachezaji wa Yanga waliendelea kuzunguka hapa na pale bila hata ya kusogea kuhoji au japo kusikiliza kinachojiri. Inawezekana formula za Ras Simba bado zikawa mgogoro kwa kiasi fulani, yumkini nina imani uwepo wa wachezaji kutoka mataifa mbalimbali kuna msaada mkubwa pindi kunapokuwa na uhitaji wa kimawasiliano. Bossou na Ioussouf Abubacar kutoka Africa Magharibi wana uwezo wa kurahisisha mawaziliano pindi mechi inapochezeshwa na waamuzi wazungumzao Kifaransa, ilhali wazimbabwe Ngoma na Kamusoko wakikimudu ‘kizungu’ ipasavyo.
Watanzania wote wanaojielewa kutoka kila pembe ya nchi hii watakuwa na kila sababu ya kuiunga mkono klabu ya Yanga. Hii ni kwa kutambua kuwa kila hatua inayopiga Yanga kuanzia hivi sasa inaliongezea Taifa alama au pointi ambazo faida yake ni ongezeko la vilabu vinavyoiwakilisha nchi katika mashindano ya kimataifa na kupata zaidi ya timu mbili kutuwakilisha.
Isiposhinda Yanga, ashinde nani?? Tusiposhinda leo, tushinde lini???
Maoni
Chapisha Maoni