Ifahamu gharama inayotumika kubomoa majengo ya TANESCO Ubungo

Zoezi la ubomoaji wa majengo yalipokuwa Makao Makuu ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) bado linaendelea, ili kupisha ujenzi wa barabara za juu (Flyover) katika eneo la makutano ya barabara ya Sam Nujoma na Morogoro, Ubungo.

Ubomoaji wa majengo hayo unatarajia kugharimu kiasi cha shilingi milioni 700, kiasi ambacho kimekuwa kikubwa kutokana na uhitaji wa kutumia mashine na vifaa vingine vya kisasa katika ubomoaji, ili kutoathiri majengo mengine yatakayobakia.

Eneo linalobomolewa linahusisha jengo la ofisi za Makao Makuu, ofisi za mapokezi, karakana pamoja na uzio wa jengo hilo.

Kwa mujibu wa Mtendaji Mkuu wa Uwekezaji wa TANESCO, Khalid James amesema kuwa, zoezi la ubomoaji limechelewa na kuwa la muda mrefu, kwa kuwa unahitajika umakini wa hali ya juu, kutokana na kuwa baadhi ya majengo hayakuathiriwa na agizo la ubomoaji lililotolewa.

“Tunabomoa tu baadhi ya majengo, na tunatakiwa kulinda majengo yanayobaki ambayo hayakuathiriwa na agizo la ubomoaji,” alisema James.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Joseph Nyamhanga ameagiza kuwa zoezi hilo la ubomoaji likamilike kufikia Februari 1, mwaka huu na kuongeza kuwa ujenzi wa barabara hiyo utaanza kabla ya kuisha kwa mwezi Februari.

“Nataka zoezi la ubomoaji likamilike kufikia Fbruari 1, mwaka huu ili kupisha ujenzi wa barabara za juu (interchange) ya Ubungo,” alisema.

“Kwa sasa wakandarasi wanahamisha baadhi ya miundombinu kama vile, umeme, mabomba ya maji, mabomba ya  gesi na nyaya za mawasiliano,” alisema.