Wakati wananchi wa Kenya wakisubiria kwa hamu tukio la kuapishwa kwa Kiongozi wa Umoja wa Vyama vya Upinzani nchini humo (NASA) Raila Odinga, Gavana wa Kaunti ya Machakos Dkt. Alfred Mutua amesema kuwa kama tukio hilo litafanikiwa kufanyika basi ni dhahiri kuwa bara la Afrika ni tundu la choo.
Dkt. Mutua amesema kuwa Kenya itakuwa nchi ya kwanza duniani kuapisha marais wawili katika awamu moja.
“Kama hili la kuapishwa kwa kiongozi wa NASA litafanikiwa basi utakuwa mfano mzuri utakaodhihirisha kuwa bara letu ni mfano wa Tundu la Choo. Mtu utawezaje kuapishwa wakati huo huo kuna kiongozi mwingine ameshaapishwa na Jaji Mkuu? hii ni aibu kwa bara letu,“ameandika Dkt. Mutua kwenye ukurasa wake wa Twitter.
Neno ‘Tundu la Choo’ limewa maarufu zaidi duniani baada ya Rais Donald Trump wiki mbili zilizopita kutamka nchi za Afrika na Haiti ni mfano wa ‘Tundu la Choo’.
Kiongozi huyo wa upinzani nchini Kenya anatarajiwa kuapishwa Januari 30, 2018 na kuwa Rais wa watu wengi kama anavyojiita.