Mabingwa watetezi wa ligi kuu Tanzania bara wamebanwa na kulazimishwa suluhu kwenye uwanja wa Uhuru na kikosi cha Mtibwa Sugar kutoka Turiani, Morogoro.
Ni mechi ya tatu Yanga wanatoka sare katika ligi ikiwa ni mechi ya tano tangu kuanza kwa ligi msimu huu. Wanajangwani walitoka sare kwa mara ya kwanza dhidi ya Lipuli kwenye mechi ya ufunguzi walipolazimisha sare ya kufungana 1-1.
Mara ya pili Yanga kutoka sare kwenye mchezo wa ligi ilikuwa mechi dhidi ya Majimaji FC ugenini kwenye uwanja wa Majimaji mkoani Ruvuma walipolazimisha matokeo ya kufungana 1-1.
Yanga wameshinda mechi mbili kati ya tano walizocheza, walishinda 1-0 ugenini dhidi ya Njombe Mji halafu wakapata ushindi wao wa pili dhidi ya Ndanda FC kwenye uwanja wa Uhuru.
Kikosi cha Mtibwa kimepata sare ya pili mfululizo ugenini, mechi yao ya kwanza kupata sare walitoka 1-1 dhidi ya Ruvu Shooting kwenye uwanja wa Mabatini, Mlandizi.
Kiungo Pius Buswita amecheza kwa mara ya kwanza tangu aliposajiliwa na Yanga na uhamisho wake kugubikwa na mvutano kwamba amesaini vilabu viwili tofauti.
Yanga na Mtibwa zimecheza kwa mara ya kwanza bila kufunga, mechi zao zote zilizopita zilimalizika huku timu hizo zikifanikiwa kufunga magoli hata walipotoka sare ilikuwa ni ya magoli.