Ikiwa nimuda wa wiki tatu umepita tokea kushambuliwa kwa risasi Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Antipas Lissu huko Dodoma majira ya mchana alipokuwa akitoka Bungeni kuelekea nyumbani kwake, serikali sasa imetangaza kuanza mchakato wa kuboresha ulinzi kwa wabunge wote.
Hayo yalisemwa jana na Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi, Mwigulu Nchemba, alipokuwa akizungumza katika kipindi cha runinga cha Clouds360 kinachorushwa na Clouds TV.
Waziri Nchemba alieleza kuwa maswala ya ulinzi kwa viongozi wa umma yapo kwa mujibu wa sheria, lakini kuna watu ambao bado hawajatambulika na kupewa ulinzi.
Aliendelea kwa kusema kuwa suala la ulinzi kwa wabunge linafanyiwa kazi na ulinzi utaongezwa.
“Kwa sasa suala hilo la ulinzi kwa waheshimiwa wabunge linashughulikiwa na tutaongeza ulinzi kwenye maeneo yote ya viongozi na kufanya doria za mara kwa mara,”alisema Mwigulu.
Waziri aliwataka wananchi wote kuwa na amani na kuondoa hofu dhidi ya matukio ya kihalifu yaliyotokea na kueleza kuwa vyombo vya ulinzi na usalama nchini vinafanya kazi yake ya kuhakikisha vinawakamata na kuwatia hatiani wae wote wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu.