Fahamu kiwango cha fedha ambacho ukisafiri nacho lazima utoe taarifa TRA

Mamlaka wa Mapato Tanzania (TRA) ambayo ndiyo yenye dhamana ya kusimamia masuala mbalimbali yahusuyo fedha imetangaza kuwa, kuanzia Oktoba Mosi mwaka huu, mtu yeyote akisafirisha fedha taslimu dola za kimarekani 10,000 ambazo ni sawa Tsh 22.5 milioni ni lazima awe amejaza fomu yenye maelezo kuhusu fedha hizo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kaimu Kamishna wa Forodha na Ushuru wa Bidhaa, George I. Mnyitafu imeeleza kuwa TRA imepata mamlaka hayo kutokana na Sheria ya Kudhibiti Fedha Haramu, Sura 423 na Kanuni yake inayohusu utoaji wa taarifa ya kiasi cha fedha taslimu na Hati za Malipo zinazosafirishwa kuingia au kutoka nchini.

Sheria hiyo imeipa Mamlaka ya Mapato Tanzania mamlaka ya kusimamia utoaji wa taarifa kuhusu fedha zinazosafirishwa kuingia au kutoka nchini.

Taarifa hiyo ya TRA inahusu usafirishaji wa fedha taslimu au hati za malipo (Bearer Negotiable Instruments) zinazofikia au kuzidi dola za kimarekani 10,000 (elfu kumi) au fedha nyingine yoyote yenye thamani sawa na hiyo iwapo fedha au hati hizo zitasafirishwa kwa njia
zifuatazo;

(a) mtu yeyote anayesafiri akiwa nazo au katika mizigo anayoambatana nayo au katika chombo cha usafiri;
(b) katika makontena ya kubebea mizigo, na
(c) kwa njia ya vifurushi.

TRA imeutaarifu umma kuwa, kuanzia tarehe 01 Oktoba 2017, msafirishaji yeyote wa fedha taslimu au hati za malipo zinazofikia kiwango kilichotajwa na kanuni hizi atalazimika kutoa taarifa kwa kujaza fomu zitakazopatikana kwa maafisa forodha mipakani.

Mamlaka hiyo imesisitiza kuwa, kutotoa taarifa au kutoa taarifa zisizo sahihi kuhusu usafirishaji huo fedha au hati za malipo ni kosa kisheria.

Kuwatoa hofu wananchi kuhusu sheria hii, TRA imeeleza kwamba, utaratibu huu haukusudii kuzuia usafirishaji wa fedha taslimu na hati
za malipo kuingia au kutoka nchini.

Kwa taarifa au ufafanuzi zaidi tafadhali wasiliana na Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa namba za simu za bure: 0800 750075 au 0800 780078, au Barua pepe: huduma@tra.go.tz