Simba SC haijawahi kuifunga Mwadui FC katika VPL…
Na Baraka Mbolembole
Jamhuri Kiwhelo ‘Julio’ ndiye kocha aliyeipandisha ligi kuu Tanzania Bara timu ya Mwadui FC ya Shinyanga, Februari 2015 tena wakiwa mabingwa wa ligi daraja la kwanza.
Akiwa ni mwanachama, mchezaji na kocha wa zamani wa Simba SC baadhi ya mashabiki wa kandanda nchini waliamini itakuwa rahisi zaidi kwa Mwadui FC kupoteza game vs Simba, huku wengine wakiamini Yanga SC itakuwa na kazi kubwa zaidi watakapokutana na timu hiyo ya Shinyanga.
Kweli, Yanga ilitangulia kucheza na Mwadui FC pale Kambarage Stadium msimu uliopita na walikutana na game yenye ugumu wa kiwango cha juu. Licha ya Donald Ngoma kutangulia kuifungia timu yake, Paul Nonga akasawazisha kabla ya kumalizika kwa kipindi cha kwanza.
Mzimbabwe huyo akafunga goli la pili lakini dakika tatu kabla ya kumalizika kwa mchezo, mshambulizi mkongwe, Bakar Kigodeko akaisawazishia tena Mwadui FC na kutengeneza sare ya kufungana 2-2.
Yanga ilishinda 2-1 katika game ya marejeano jijini, Dar es Salaam baada ya kupambana na kusawazisha goli la uongozi.
Desemba 15 mwaka uliopita, Julio aliiongoza Mwadui FC kwa mara ya kwanza vs Simba na matokeo yalikuwa sare ya kufungana 1-1.
Mei 8, 2016 katika uwanja wa Taifa, Dar es Salaam goli pekee lililofungwa na mshambuliaji, Jamal Mnyate (sasa yupo Simba) liliwapa Mwadui ushindi wa goli 1-0 na baada ya kumalizika kwa mechi, Julio alicheza sana aina ya muziki anaoujua yeye mwenyewe ili kuonesha namna alivyofurahia ushindi huo.
JULIO HAYUPO
Kocha huyo mwenye maneno mengi alibwaga manyanga katika timu hiyo kwa sababu tu haridhishwi na uchezeshaji wa waamuzi katika soka la Tanzania. Jumamosi hii Mwadui FC wataikaribisha Simba katika mchezo wa raundi ya 12.
Simba inaongoza ligi ikiwa na alama 29 baada ya kucheza game 11 wakati Mwadui FC ipo nafasi ya kumi ikiwa na pointi 13.
Safu ya ulinzi ya Mwadui imeruhusu magoli kumi na ile ya mashambulizi imefunga magoli tisa tu. Simba upande wao wamefanikiwa kufunga jumla ya magoli 21 na kuruhusu magoli matatu katika nyavu zao.
Wakati Mwadui ikiwa chini ya Julio timu hiyo haikuwahi kupoteza mchezo dhidi ya Simba, itaendeleza rekodi yake?
Maoni
Chapisha Maoni