NABII ADAM (A.S): MWANZO WA MWANADAMU NA HISTORIA YA KWANZA YA MAISHA|T MEDIA NEWS
Allah (S.W) ndiye Muumba wa kila kitu. Kiumbe cha kwanza kuumbwa kilikuwa ni Qalam, ambacho Allah alikiumba ili kuandika yote yatakayofanywa na viumbe—mema na maovu. Baadaye akaumba Lauhul-Mahfudh na viumbe vingine vyote, pamoja na mbingu saba na ardhi katika siku sita. Kabla ya kuumbwa kwa Nabii Adam (A.S), Allah alikuwa amewaumba majini. Hawa walifanya uharibifu mkubwa duniani na kumwaga damu. Kutokana na hali hiyo, Allah aliwatuma malaika kuwaangamiza. Katika tukio hilo, alibaki jini mmoja aliyeitwa Iblis (Azazil), ambaye kwa sababu ya ibada yake nyingi, alipewa nafasi ya kuishi pamoja na malaika. KUUMBWA KWA ADAM (A.S) Allah alipowajulisha malaika kuwa ataumba kiumbe kipya duniani, walishangaa wakasema: “Je, utaweka humo atakayefanya uharibifu na kumwaga damu, wakati sisi tunakusifu na kukutukuza?” Allah akawajibu: “Hakika mimi najua msiyoyajua.” Kisha Allah akamuumba Adam (A.S) kwa udongo wa aina mbalimbali, akamfinyanga mpaka akawa katika umbo kamili la binadamu. Baada ya muda, ...