MAHAKAMA ya Rufaa nchini Marekani imekataa kuirudisha tena marufuku iliyowekwa na Rais Donald Trump ya wasafiri kutoka nchi saba za kiislamu na wakimbizi wote kuingia nchini humo.
Jopo la majaji watatu kwa kauli moja limekataa kuupindua uamuzi uliotolewa na Jaji kutoka mji wa Seattle, ambaye wiki iliyopita alizua sehemu za amri iliyotolewa na Rais huyo wa Marekani.
Habari zinasema uamuzi huo kwa sasa utapelekwa katika Mahakama ya Juu.
Muda mfupi tu baada ya uamuzi huo wa mahakama kutangazwa, Rais Donald Trump aliwaambia waandishi wa habari kwamba ana uhakika mwisho wake ataibuka mshindi.
“Ni uamuzi wa kisiasa na tutakwenda kukutana mahakamani, na natarajia kufanya hivyo, hali ya usalama nchini mwetu iko hatarini na ni hali mbaya sana,” alisema Trump anayetaka raia wa nchi za Somalia, Libya, Syria, Iraq, Sudan, Iran na Yemen wasiruhusiwe kuingia Marekani, kwa kile anachoamini raia wa nchi hizo ni hatari kwa usalama wa nchi hiyo.
Katika hatua nyingine Rais Trump ametangaza mfululizo wa amri za Rais kwa lengo la kupunguza uhalifu.
Akizungumza wakati wa kuapishwa kwa Mwanasheria Mkuu wa nchi hiyo, Rais wa Marekani alisema uhalifu umeongezeka nchini Marekani na utawala wake utalishughulikia suala hilo kuanzia sasa.
Amri hizo zilizotangazwa ni pamoja na kukabiliana na magenge ya wafanyabiashara ya dawa ya kulevya na wafanyabiashara za uhalifu.